Wanafunzi 100 Bara, Zanzibar waelimishwa usalama barabarani

Mwalimu wa Shule ya Msingi Nguzo Mbili wilayani Geita Tunu Mjema (kulia) akipokea kikombe cha ushindi kutoka Mgeni rasmi kutoka Ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa wa Geita Masumbuko Stephano (kushoto) baada ya shule hiyo kuibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya kuchora mchoro wa usalama barabarani kwa shule tano zilizoshiriki shindano hilo mkoani Geita.

Muktasari:

  • Zaidi ya wanafunzi 100,000 wa shule za msingi 100 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Ruvuma, Dodoma na Zanzibar wamejengewa uwezo elimu ya usalama barabarani.

Geita. Zaidi ya wanafunzi 100,000 wa shule za msingi 100 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Ruvuma, Dodoma na Zanzibar wamejengewa uwezo elimu ya michoro ya usalama barabarani ili kukabiliana na ajali za mara kwa mara.

Hayo yalielezwa leo Oktoba 20 na mwakilishi wa mkurugenzi mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Ambokege Minga wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa wanafunzi walioshinda shindano la kuchora michoro ya usalama barabarani lililofanyika shule ya msingi Kalangalala mkoani hapa.


Mlinga ambaye ni ofisa usalama wa barabarani na mazingira wa Puma, alisema mpango wa kuwajengea uwezo wanafunzi kuhusu usalama wa barabarani ulizinduliwa miaka tisa iliyopita na jumla 100 zilinufaika kwa kupewa mafunzo ya usalama barabarani kwa nyakati tofauti.


“Lengo kubwa la mpango huu ni kuwafanya watoto kuwa na uelewa wa masuala ya usalama wa barabarani wakiwa wadogo. Pia kujua matumizi bora ya barabara mbalimbali,” amesema Mlinga.


Mlinga alisema katika mkoa wa Geita, jumla ya wanafunzi 12,000 walinufaika na mpango huo kutoka shule tano za msingi za halmashauri ya mji wa Geita. Alisema mafunzo hayo yalikwenda sambamba na utoaji wa zawadi walioshinda katika mchakato huo.


 “Tumeamua kuja Geita kwa sababu ni mji unaokua na shughuli za kijamii na ongezeko la watu wenye magari yanayohatarisha usalama wa watoto wanaokwenda shuleni na kurudi nyumbani. Hadi sasa tumewafundisha wanafunzi 12,000 katika shule tano za Geita Mji,” amesema Mlinga.


Mkaguzi wa polisi kikosi cha usalama barabarani wilayani, Geita Emmanuel shagaya amewaomba wanafunzi waliopata mafunzo kufikisha ujumbe unaohusu usalama barabarani kwa wenzao na wazazi wao.


"Mkifika nyumbani waiteni wazazi wote, waambieni wazingatie usalama wao wakiwa barabarani.Tukifanya hivyo tutakuwa salama na tutapunguza ajali za barabarani zitapungua na kuokoa Taifa.


Naye Ofisa Elimu mkoa wa Geita, Masumbuko Magang'bila aliwashukuru Puma kwa kupeleka mafunzo hayo mkoani humo akisema yatasaidia kuokoa maishja ya watu.


"Tunapotoa mafunzo kwa wanafunzi maana yake tunakwenda kupeleka elimu hiyo ngazi ya chini kabisa, wanafunzi ambao tunawaona shuleni wana wazazi na walezi wao ndio sisi." alisema.


Katika shindano hilo, zawadi kubwa ilikuwa Sh4 milioni kwa shule itakayotoa mshindi wa kwanza itatoa hamasa kwa shule kuwa mabalozi wazuri, Sh 500,000 kwa mwanafunzi atakayechora vizuri. Shule ya Nguzo Mbili ndio iliyoibuka kidedea katika shindano hilo.