Wanafunzi 2,162 hawajaripoti shule mkoani Lindi

Sunday March 07 2021
wanafunzi pic
By Mwanja Ibadi

Lindi. Wanafunzi  2,162 sawa na asilimia 13  ya wanafunzi 15,860 waliochaguliwa kuendelea na sekondari mkoani Lindi mwaka 2021 hawajaripoti katika shule walizopangiwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro.

Hayo yameelezwa na ofisa elimu Mkoa wa Lindi, Victor Kayombo katika mahojiano na Mwananchi Digital.

Amesema hadi Februari 26, 2021 walikuwa hawajaripoti  katika shule walizopangiwa na kati yao wasichana ni 1,157 na wavulana 1,005.

Akitaja halmashauri ambazo wanafunzi hawajaripoti na idadi yao kwenye mabano amesema Kilwa (481), Nachingwea (452), Mtama (390), Ruangwa (353), Liwale (292) na Lindi manispaa (194).

Kayombo amesema hadi Februari 26, 2021 wanafunzi walioripoti shule walizopangiwa ni 13,495, na kati yao wasichana ni  6,945 na wavulana 6,753 sawa na asilimia 87.

Amesema kutokana na hali hiyo  baadhi ya wazazi na walezi wameanza kuchukuliwa hatua lakini hakuzitaja.

Advertisement


Imeandikwa na Mwanja Ibadi

Advertisement