Wanafunzi 26 wahitimu mafunzo GGML

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imewaaga wahitimu 26 wa mafunzo tarajali waliokuwa wakifanya mafunzo katika kampuni hiyo kwa mwaka 2021/2022.

Dar es Salaam. Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imewaaga wahitimu 26 wa mafunzo tarajali waliokuwa wakifanya mafunzo katika kampuni hiyo kwa mwaka 2021/2022.


Kampuni hiyo huwa inatekeleza programu ya mafunzo tarajali kila mwaka kwa kushirikiana na ofisi ya waziri mkuu inayohusika na ajira, vijana, na watu wenye ulemavu pamoja na Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na Chama cha Waajiri Nchini (ATE).


Hii ni mojawapo ya mkakati wa kampuni hiyo kunufaisha jamii ya Tanzania kutokana na shughuli za uchimbaji dhahabu.


Wahitimu hao wameagwa hivi karibuni katika hafla iliyofanyika mkoani Geita ambapo Meneja Mwandamizi anayesimamia kitengo cha afya, Usalama, Mazingira na Mafunzo kutoka GGML, Dk Kiva Mvungi aliwapongeza wahitimu hao kwa kufikia hatua hiyo muhimu katika fani walizozisomea.


“Tunawapongeza kwa kupata fursa hii. Kampuni yetu imekuwa ikitoa nafasi hizi kila mwaka na wahitimu wengi wa vyuo vikuu wamekuwa wakituma maombi yao. Kwa ambao mlichangamkia fursa za ajira zilipotangazwa, tunawapongeza kwa kuwa wafanyakazi wa kudumu wa kampuni hii. Kwa ambao bado hamjapata ajira, endeleeni kutuma maombi yenu kila GGML inapotoa nafasi za kazi,” alisema


Dk Mvungi alisema kukamilisha programu hii ni mwanzo sasa wa kuonesha ukomavu wenu mnapoitwa katika udahili wa kazi.


Alisema asimilia kubwa ya vijana waliopitia programu hiyo wameajiriwa na kampuni mbalimbali, “bila shaka nanyi mtaajiriwa pia hapa GGM au kwingineko. Lengo letu ni kuhakikisha sekta ya madini hapa nchini inapata wafanyakazi wenye uzoefu,” alisema


Naye

Mhandisi Ruth Mugurusi ambaye ameajiriwa katika kitengo cha ulipuaji cha GGML alishukuru kupata fursa hiyo akiwa katika mchakato wa kuhitimu mafunzo yake.


“Mimi ni Mtanzania ambaye naishukuru sana GGML kwa kunipatia fursa hii. Baada tu ya kuhitimu masomo yangu ya chuo kikuu, nilituma maombi na kuanza mafunzo haya. Namshukuru Mungu nikiwa katika kipindi cha mafunzo haya, zilitangazwa nafasi na mimi na wenzangu tukatuma maombi na kufaulu usaili na leo hii hatimaye tumeajiriwa na GGML.”


“Nawashauri wahitimu wengine wa mafunzo haya, waendelee kutuma maombi yao kila nafasi zinapotangazwa kwa kuwa kampuni hii ni kampuni inayotoa fursa kwa watu wote wakiwemo wanawake,” alisema Mhandisi Mugurusi.


Tangu programu hii ianze mwaka 2009 hadi hivi sasa wahitimu 168 wamenufaika ambapo kati ya hao wasichana ni 58 na wavulani ni 110.  Asilimia kubwa wameajiriwa na GGML katika vitengo vya uchenjuaji dhahabu, uhandisi, ufundi, ulipuaji na uchimbaji madini na baadhi yao wameajiriwa katika makampuni mengine ndani na nje ya nchi.