Wanafunzi tisa waliomkashifu Ruto waachiwa

Saturday August 06 2022
wanafunzii
By Mwandishi Wetu

Nairobi. Wanafunzi tisa wa Chuo Kikuu cha Moi waliokamatwa na kushtakiwa kuhusiana na kusambaza maandishi ya chuki katika kundi la WhatsApp wameachiwa kwa dhamana ya Sh1 milioni au dhamana ya fedha taslimu Sh500,000 kila mmoja.
 Wanafunzi hao wanatuhumiwa kwa kueneza habari za uwongo ili kujenga hofu kabla ya  Uchaguzi  Mkuu utakaofanyika Agosti 9, 2022.

Katika shtaka la kwanza, Ronald Odhiambo Ochieng, Martin Rodgers, Josphat Chacha, Ian Muibanda, Brian Kipkorir Keter, Dennis Salim Wakhanya, Beatrice Wangari Kumari, Samuel Otieno na Ann Aoko walishtakiwa kwa kuchapisha habari za uongo, kinyume cha Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandao ya mwaka 2018.
 Mahakama ilielezwa kuwa Julai 29 katika Chuo Kikuu cha Moi, katika kaunti ndogo ya Kesses huko Uasin Gishu, kwa pamoja na wengine ambao hawakuwa mahakamani, walichapisha habari za uwongo kwa kutumia simu zao za mkononi na kusababisha hofu na wasiwasi miongoni mwa Wakenya.
 Habari hizo ziliionya jamii fulani kuondoka Uasin Gishu kabla ya uchaguzi wa wiki ijayo, ikiwa hazikupanga kumpigia kura mgombea fulani wa kiti cha rais.
 Waendesha mashtaka waliiambia mahakama kwamba habari katika taarifa hizo zilikusudiwa kusababisha hofu, fujo na vurugu miongoni mwa wananchi.
 Wanadaiwa kutumia taarifa za uongo kujenga hofu ili kushawishi upigaji kura, kinyume cha Sheria ya Makosa ya Uchaguzi ya 2016.
 Walikanusha mashtaka mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Mogire Onkoba.
 Wanafunzi hao ambao hawakuwakilishwa na mawakili, waliiomba mahakama kuwaachia kwa masharti nafuu ya dhamana.
 “Ninatoka katika familia maskini. Nawategemea wazazi wangu, ambao wanapata shida kunilipia karo na hawataweza kunilipia bondi kubwa,” mmoja wa washtakiwa aliiambia mahakama.
 Wakili wa Serikali, David Fedha hakupinga kuachiwa kwao kwa dhamana. Lakini aliitaka mahakama itoe  masharti magumu ya dhamana kutokana na aina ya uhalifu.
 “Serikali imekuwa na upole kwa washtakiwa kwa sababu ni wanafunzi. Ndiyo maana sijapinga kuachiwa kwao kwa dhamana,” alisema.

Advertisement