Wanafunzi wa kike kunolewa programu za kompyuta

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wakazi wa Kagera waishio jijini Dar es Salaam ambao wanaunda Taasisi ya Kagera Development Foundation (Kadefo).

Muktasari:

  • Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wana-Kagera kuungana kwa ajili ya maendeleo ya mkoa.

Dar es Salaam. Wakazi wa Mkoa wa Kagera waishio Dar es Salaam wamepanga kuwafundisha kutengeneza programu za kompyuta (Coding) wanafunzi wa sekondari mkoani humo ili kuendana na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Mpango huo unawalenga wanafunzi wa kidato cha nne na cha sita ili kuwajengea uelewa na ujasiri katika matumizi ya teknolojia ya habari kupitia ufundishwaji wa somo la python ambayo ni lugha maalumu kwa ajili ya kutengeneza programu.

Mwenyekiti wa taasisi ya Kagera Development Foundation (Kadefo), Erick Kamuzora amesema kuanzishwa mafunzo hayo ni moja kati ya mambo yanayolenga kuwainua wanawake katika upande wa teknolojia ambao wanaonekana kuachwa nyuma.

“Kwa kushirikiana na mwenzetu anayeishi nchini Marekani, tulianzisha mafunzo ya Coding kupitia mtandao kwa ajili ya wasichana, tulifanya majaribio,” amesema Kamuzora.

Wanafunzi wa kike kunolewa programu za kompyuta

Katibu Mkuu wa Kadefo, Tryphon Rutabanza, amesema wakati wa majaribio ya mafunzo hayo, wanafunzi 24 walifundishwa na baada ya kuhitimu wapo walioajiriwa na wengine waliendelea na shule.

“Lengo hasa ni wale wanaeondelea waweze kumudu masomo na programu mbalimbali huko mbele, awali tulilenga wasichana lakini sasa tumeamua kuweka mchanganyiko baada ya mwamko kuwa mdogo,” amesema Rutabanza.

Amesema awali wakati wanafanya majaribio, aliyekuwa akisimamia ni mkazi wa Kagera anayeishi Marekani lakini waliamua kuwafundisha vijana wengine wawili kwa ajili ya kufuatilia mafunzo kwa vitendo.

“Nafikiri Juni tutaanza tena, tutashirikiana na Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa (Carumuco), wanafunzi tunawapata kupitia matangazo shuleni na kwa wazazi, kwa sababu kipaumbele chetu ni wasichana wao wanapewa punguzo la ada,” amesema.

Mbali ya hayo, Kamuzora amesema mkoa huo umebaki nyuma kwa vigezo vingi vya maendeleo, ikiwemo uendelezaji wa viwanda, idadi ya kaya zenye vyoo, maji, lishe duni, miundombinu duni na chakavu ya shule za msingi.

“Ukitaka kujua kwa nini tunakwama kimaendeleo, chukua kioo ujiulize je, ninayemuona ndani ya kioo ndiye anayetukwamisha, kama si wewe ni kitu gani unafanya kukwamua, hatuna sababu ya kutafuta mchawi, wewe na mimi tunahusika na mkwamo,” amesema Kamuzora.

Amesema ikifika siku wakaamua mmoja mmoja kufanya jambo kwa ajili ya mkoa, maendeleo yataanza kupatikana kama vile yalivyo matamanio yao.

Amewataka watu wenye ushawishi kutumia nafasi zao kuusaidia Mkoa wa Kagera ili kuimarisha uchumi.

“Wale walio nje ya nchi, wekezeni nyumbani ili kuongeza kiwango cha ukwasi kwa familia zenu maisha yao yaimarike na kuwa bora,” amesema Kamuzora.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliyekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo wa wazaliwa wa Kagera waishio Dar es Salaam, amewataka wana-Kagera kuungana ili wasipoteze nguvu na ubunifu wanaoweza kuuratibu pamoja.

“Tuwe ndani ya nchi, nje ya nchi tufike mahali tuamue kuwa lazima tuungane tusukume maendeleo ya mkoa wetu,” amesema.