Wanafunzi wadai kumshuhudia mwalimu akiiba kompyuta

Saturday March 06 2021
mwalimu pic
By Fina Lyimo

Moshi. Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Okaoni Wilaya ya Moshi wamedai walimshuhudia mwalimu wao,  Akibary Hema akiiba kompyuta mpakato mali ya shule hiyo.

Kaimu Kamanda  wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona, ameeleza hayo leo Jumamosi Machi 6, 2021 na kwamba mwalimu huyo alikamatwa Machi 4, 2021 akibainisha kuwa mwalimu huyo anashikiliwa na polisi.

“Wanafunzi walimuona akiiba kompyuta hiyo na kutoa taarifa kwa mkuu wa shule. Pia, mwalimu mkuu na walimu wengine walimsihi airejeshe lakini hakutaka kusikia ndipo walipoamua kwenda kumpekua kwenye chumba chake na kuikuta kompyuta hiyo,” amesema akibainisha kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Moshi, Moris Makoi amesema  mwalimu huyo anadaiwa kuchukua kompyuta hiyo na kuificha katika chumba anachoishi katika kata ya Arusha Chini.

"Baada ya kupata taarifa hizo tulishirikiana na uongozi wa kata kwenda kumpekua katika chumba anachoishi na tuliikuta hiyo kompyuta mpakato," amesema Makoi na kusisitiza kuwa walimu wenzake walimsihi kuirejesha kompyuta hiyo lakini hakutaka kuwasikiliza.

Advertisement