Wanafunzi wenye ulemavu wa kutosikia wapewa msaada kuchochea uandishi vitabu

Muktasari:

Msaada huo umehusisha fulana maalumu za ‘Mjue Mtunzi’ pamoja na kalamu kama kielelezo cha kutoa motisha katika tasnia ya uandishi vitabu nchini.

Dar es Salaam. Wanafunzi 32 viziwi katika Shule ya Msingi Maweni iliyopo wilaya ya Kigamboni wamekabidhiwa vifaa vya shule ili kuwapa motisha ya kuendelea kujifunza.

Shughuli hiyo ya kukabidhi vifaa vya shule imefanyika leo Alhamisi Juni 30, 2022 jijini hapa na waandaaji wa tamasha la “Elite Mjue Mtunzi” wakiongozwa na mwandishi wa riwaya nchini, Laura Pettie akiwa pamoja na wadau wengine wa tamasha hilo, Hussein Molito, Kado Cool, Kalunga Matovolwa na Abubakar Ufunguo.

Shughuli hiyo ilihusisha ugawaji wa fulana maalumu za ‘Mjue Mtunzi’ pamoja na kalamu kama kielelezo cha kutoa motisha katika tasnia ya uandishi vitabu nchini.

“Uwaridi kupitia ‘Elite Mjue Mtunzi’ tunaamini katika ushirikishaji wa makundi maalumu katika harakati za kukuza tasnia. Tumekuja hapa kuwapa kalamu ili waandike, wao wametupatia lugha ya alama ili tuwasiliane. Tumewaona watunzi wenye ndoto na wasomaji vitabu wa baadaye kupitia watoto hawa,” amesema Pettie.

Wakizungumza kwa kutumia lugha ya alama, baadhi ya wanafunzi; Banoga Maduwa na Victoria Andrea wameonyesha furaha yao baada ya kupokea zawadi hizo kutoka kwa waandishi.

Mwalimu wa darasa la viziwi, Fatuma Selemani amesema anawashukuru waandishi wa vitabu kwa kuwatambua watoto viziwi kwasababu ni kundi ambalo limesahaulika. Amesema wameonyesha mwanga kwa watoto hao na kuwapa hamasa ya kuendelea kusoma zaidi ili nao wanatamani kufikia hatua hiyo.

Tamasha la “Elite Mjue Mtunzi” lililodhaminiwa na kampuni ya Elite Bookstore, linatarajia kufanyika Julai 3 mwaka huu katika ukumbi wa NSSF Ilala Boma. Tamasha hilo litawaleta pamoja waandishi wa vitabu nchini pamoja na wasomaji.

Tamasha hilo linalohamasisha utunzi na usomaji wa vitabu litafanyika kwa mara ya pili jijini Dar es salaam chini ya uongozi wa Umoja wa Waandishi wa Riwaya wenye Dira (Uwaridi).

Mgeni rasmi katika tamasha hilo anatarajiwa kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.