Wananchi 33 wanusurika kifo kwa kula kibudu

Baadhi ya wananchi waliokula kibudu kijiji cha Laalalaa katabya Namelock na kudhurika wakiwa duka la dawa hapo kijijini kununua dawa kuokoa maisha yao baada ya kushindwa na gharama za kukodi gari kwenda hospitali ya wilaya ya Kiteto. Picha na Mohamed Hamad Kiteto

Muktasari:

  • Kwa kawaida kilo moja ya nyama inauzwa Sh8,000 lakini wao walinunua kwa Sh2,000 na kula.

Kiteto. Watu 33 wa Kijiji cha Lalalaa, Kata ya Namelock wilayani Kiteto mkoani Manyara, wamenusurika kifo baada ya kula mzoga wa nyama ya ng'ombe ambayo haijapimwa.

Wakizungumzia sakata hilo baadhi ya wahanga hao wa tukio wamesema, awali walihakikishiwa kuwa nyama hiyo ni salama wakati wanauziwa.

Akizungumzia sakata hilo jana Machi 6, 2023, Pima Peter ambaye ni mwathirika alisema, alinusurika kifo baada ya kula nyama hiyo na  kupatiwa tiba ya haraka ya kuongezewa maji hapo kijijini kufuatia kuzidiwa na sumu ya nyama hiyo aliyokula.

"Nilikuwa naharisha na kutapika, nilikata tamaa kwa hali niliyokuwa nayo...kwani hata hao waliokuwa wananipa huduma ya kwanza sijawatambua kabisa," alisema Pima.

Alisema mara nyingi huwa hapo Kijijini wanauziwa nyama ambayo imetundikwa juu ya mti na wamezoea hivyo, lakini walishangaa siku hiyo kilo moja ya nyama iliuzwa shilingi 2,000 badala ya 8,000 bei ambayo imezoeleka

Kwa upande wake Mariamu Isa alisema alipatwa na ugonjwa wa kuharisha na kutapika yeye na watoto wake watano na hali yao sasa inaendelea kuimarika.

"Kwa kweli kilikuwa ni kifo chetu...Mimi na watoto wangu watano tulipatwa na ugonjwa wa kuharisha na kutapika, nilijua kuwa ndio mwisho wa maisha yetu lakini nashukuru Mungu mpaka sasa hali yangu inaendelea kuimarika mpaka mchana huu nimeharisha mara nne tu," alisema.

Diwani wa Kata ya Namelock, Masio Kibiki amesema awali baada ya kuona madhara hayo yanaendelea kujitokeza alitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga ambaye alimwagiza wagonjwa wapelekwe Hospitali ya Wilaya ya Kiteto lakini ilishindikana kutokana na kutokuwa na fedha za kukodisha gari.

"Ujue waliopatwa na hili tatizo walikuwa 33 kipato chao ni duni sana, sasa ililazimika tuwapeleke duka la dawa na kununua drip ili watundikiwe huko nyumbani kwao," alisema Diwani Kibiki.

"Nilipompigia tu mkuu wa wilaya aliniagiza niwambie waende Hospitali ya Wilaya ya Kiteto nikalazimika kutoa taarifa nyumba kwa nyumba. Nikakuta baadhi yao wameondoka na wengi wao walibaki hapa ambapo walilazimika kupatiwa dripu kwa kununua wenyewe kwenye duka la dawa hapa kijijini.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mbaraka Batenga amekiri watu hao 33 wa kijiji hicho kuathirika kwa kula nyama hiyo ya ng'ombe ambayo haijapimwa na kuonya wananchi hao kuacha kula nyama ambayo haijapimwa.

 "Mtu yeyote anayetaka kuchinja mfugo wake lazima upimwe, hapa kijijini kuna wataalamu ambao wanajukumu hilo na kuongeza kuwa watu wasile nyama ambayo haijapimwa kwani kutofanya hivyo madhara yanaweza kuendelea kujitikeza," amesema.