Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi 56,000 kunufaika mradi wa maji ifikapo Juni

Kamati ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rombo wakiwa kwenye majadiliano wakati walipotembelea miradi ya maji ya Njoro11 na Wona-Marangu wilayani humo. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rombo, kimemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Wona-Marangu, ambao utahudumia wananchi 56,000 wa Tarafa nne kuongeza kasi na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Rombo. Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro  kimemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Wona-Marangu, ambao utahudumia wananchi 56,000 katika vijiji 41 vya wilaya hiyo kuongeza kasi na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Rombo, Antony Tesha wakati alipoambatana na kamati ya siasa ya wilaya hiyo, kutembelea na kukagua miradi ya maji ya Njoro 11 na Wona-Marangu ambayo inatekelezwa katika wilaya hiyo.

Mradi wa maji wa Wona-Marangu, ambao utagharimu Sh2.9 bilioni utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 15 za maji kwa sekunde ambapo utapunguza upungufu wa maji katika wilaya hiyo kwa asilimia 30.

"Wanachi hawa wa Rombo, wana shauku kubwa ya kuona haya maji yanayotokana na hii miradi yetu. Hivyo tunamtaka mkandarasi pamoja na watendaji wakuu wanaosiamamia hii miradi ya maji, wahakikishe miradi hii inatekelezwa kwa wakati, wananchi wana shauku kubwa ya kuona, kwani kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto ya maji," amesema.

Tesha, ameipongeza serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wanatoa fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika wilaya hiyo na kusema changamoto kubwa iliyopo katika wilaya hiyo ni maji.

"Kwa hiki kinachofanyika sasa tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu, Samia Suluhu Hassan tumepata fedha za kutosha, lakini tunampongeza waziri wetu wa maji pamoja na mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda kwa kuweka msukumo mkubwa kwenye miradi hii ya maji," amesema.

"Tunaamini miradi hii itakamilika kwa wakati na watu wetu watapata maji ya uhakika, na sisi kama chama tutaendelea kutoa msukumo kuhakikisha yale tuliyoyaahidi wakati wa kampeni yanatekelezeka na maji yanapatikana kwa wananchi,"amesema Tesha.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo (Rombowasa), Martin Kinabo amesema mradi huo wa maji utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia wananchi wapatao 56,000 na mpaka sasa mradi huo umeshafikia asimilia 60.

"Wananchi wategemee ifikapo Juni mwaka huu watakuwa wamepata maji kutoka katika mradi wa maji wa Wona-Marangu ambao kwa kiasi kikubwa maji haya yatakuwa na uwezo wa kuhudumia vijiji 41 katika Tarafa nne za Mengwe, Mashati, Usseri na Mkuu."

Pamoja na Mradi huo wa Wona-Marangu, amesema mradi wa maji wa Njoro11 A na  B yenye uwezo wa  kuzalisha maji lita 1,728,000 kwa siku imeanza kufanya kazi katika  baadhi ya maeneo ya mji wa Tarakea, Kibaoni na baadhi ya maeneo ya Nayeme.

Vick Damas, ambaye ni mkazi wa Nayeme "Shida ya maji ilikuwa ni kubwa, tunashukuru serikali kutuletea  huu mradi maana mwaka jana tulikuwa hatuna maji, yaani tulikotoka kulikuwa ni kugumu kulikuwa na  hali mbaya," amesema.

Joyce Mbarasi amesema, "Ninampongeza mama Samia Suluhu Hassan ametutua ndoo kichwani, ameisaidia jamii ya Warombo, Nayeme kulikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, lakini tunashukuru tangu mwezi wa Novemba mpaka sasa tuna maji."