Wananchi kunufaika na kilimo cha parachichi, makademia Njombe

Muktasari:

Wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu watua mkoani Njombe kuwekeza katika kilimo cha zao la parachichi na makademia

Njombe. Wananchi wa Mkoa wa Njombe wanatarajia kunufaika na kilimo cha parachichi na makademia kutokana na wawekezaji kutoka Falme za Kiarabu kutaka kuwekeza kwenye kilimo cha mazao hayo.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 30, 2022 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Judica Omary baada ya kufanya ziara ya kuwaonyesha mashamba wawekezaji hao ambao wana nia ya kuwekeza mkoani Njombe.

Amesema wawekezaji hao wanahitaji zaidi ya ekari laki moja ya mashamba kwa ajili ya kuwekeza katika kilimo cha mazao hayo ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele mkoani Njombe.

Amesema wawekezaji hao wameamua kuwekeza katika makademia na parachichi kwa kuwa ni mazao ambayo yanakubali zaidi kwenye maeneo ya nyanda za juu ikiwemo mkoa wa Njombe.

"Tumepokea ugeni kutoka Falme za Kiarabu ambao wamekuja kwa nia ya kuwekeza kwenye mkoa wetu wa Njombe katika mazao ya parachichi na makademia" amesema Judica.

Amewashauri wawekezaji hao pia kuwekeza katika kilimo cha matunda ya tufaha kwa kuwa yapo maeneo mengi ambayo kilimo hicho kinakubali.

Mbunge kutoka Bunge la Afrika Mashariki, Fance Mkuhi ambaye aliambatana na wawekezaji hao amesema licha ya kuwa na majukumu ya kutunga sheria bali pia wanahamasisha fursa mbalimbali ambazo zipo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema kazi yao nyingine ni kufungua milango kwa wawekezaji kutokana na kukutana nao mara kwa mara hivyo kuwaeleza fursa zilizopo katika nchi za jumuiya hiyo.

"Tunaimani hawa wawekezaji watapata ardhi kama ambavyo Serikali ya mkoa imewaonyesha na inaendelea kuwasaidia ili waweze kufanikisha hilo" amesema Mkuhi.

Mmoja ya mkulima maarufu wa zao la parachichi mkoani humo ambaye alitembelewa na wawekezaji katika mashamba yake, Steven Mlimbila amesema kitendo cha Serikali kuendelea kutafuta wawekezaji kwa ajili ya kuwekeza kwenye kilimo hicho kinawapa nguvu ya kulima zaidi kwakuwa utaongeza upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi.

"Ni jambo zuri inaonyesha ziara ya Rais huko Oman ndiyo imeleta wageni hivyo ni fursa kwa Watanzania hasa wa Njombe ambao wanataka kuwekeza kwenye zao hili la Parachichi" amesema Mlimbila.