Wananchi Shinyanga waipongeza Serikali kwa kurasimisha viwanja

Diwani wa kata ya Ngokolo Victor Mkwizu akiwahimiza Wananchi waweze kuichangamkia fursa ya kulipia hati miliki kwa wakati.

Muktasari:

  • Wananchi Shinyanga waipongeza Serikali kwa kuanzisha urasimishwaji wa viwanja na kupata hati miliki kwa gharama nafuu.

Shinyanga. Wananchi wa mtaa wa Majengo Mapya, Manispaa ya Shinyanga wameipongeza Serikali kwa kuanzisha zoezi la upimaji viwanja kwa gharama nafuu ya Sh130,000 kwa ajili ya kuwapatia hati miliki ambayo itawasaidia kukopa kwenye taasisi za fedha.

Wakizungumza kwenye kikao cha elimu ya urasimishaji wa ardhi uliofanyika katika soko la mtaa wa Majengo Mapya, wananchi hao wamesema wanaishukuru Serikali kwa kuanzisha utaratibu wa urasimishaji na kwamba gharama za upimaji ambazo ni 130,000 watailipa bila shida.

Daniel Mayenga na Frola Joseph wanaoishi katika mtaa huo, wamesema utaratibu ulioletwa ni mzuri kwani awali walikuwa wakitumia gharama kubwa, hivyo wamepata matumaini mapya watapimiwa viwanja vyao na kupatiwa hati miliki na wataweza kukopa kiurahisi na kufanya biashara ili kujiendeleza kiuchumi.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Fue Mrindoko ameunga mkono akisema, "Suala hili tumelipokea kwa nguvu zote na kwa furaha sana, kwani tunaamini wananchi wote tutalipia fedha zilizotajwa na afisa mteule wa ardhi na tutarasimishiwa makazi yetu na kupata hati miliki ambayo itasaidia hata kupata mikopo na kufanya biashara ili kujiongezea uchumi wetu.”

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ngokolo, Victor Mkwizu amesema hatau ya wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye kikao hicho ni kuonyesha kuwa walikuwa na kiu kubwa ya kupimiwa makazi yao na kuweza kupatiwa hati miliki.

"Tatizo hili limekuwa la muda mrefu lilikuwa halijatatuliwa, na hii ni moja ya mambo tuliyoahidi kwenye mikutano yetu ya kampeni, kwamba tutatatua changamoto zilizopo.

“Hivyo hili tumelitatua na mpango huu utatekelezwa kwa wakati, lakini wale waliopimiwa kwa mda mrefu wanatakiwa kwenda kuhakiki viwanja vyao katika ofisi ya ardhi kwa sababu watu wengine walitumia majina mawili tofauti na yaliyomo kwenye kadi ya kitambulisho cha Taifa," amesema Mkwizu.

Naye Afisa mteule wa ardhi manispaa ya Shinyanga Jacob Mwinuka amesema mpango wa urasimishaji unasimamiwa na wananchi wenyewe ambapo watalipia Sh130, 000 kwa ajili ya upimaji, kununulia nondo, kokoto, na kulipa vibarua.

Hata hivyo, alisema kwa maeneo la kuabudia, kama misikiti na makanisa na hoteli watalipia Sh 500,000 na gharama ya kulipia hati miliki itategemea na ukubwa wa kiwanja chenyewe.

Mwinuka amesema katika zoezi hilo hakuna mtu atakayebomolewa na wale wenye hati watabaki na hati zao hakuna atakayewagusa kwani upimaji upo kisheria.