Wananchi wajitokeza kupima kisukari, presha kumbukizi ya Ndesamburo

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Mandela Kata ya Bomambuzi Manispaa ya Moshi, kwa ajili ya kufanya vipimo vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo shinikizo la damu na kisukari.

Muktasari:

  • Tedy Khumbelle amesema magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu, yameendelea kuwatesa wananchi na wengi hubainika wakati tatizo limekuwa kubwa kwa kuwa hawana utaratibu wa kuchunguza afya.

Moshi. Magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Shinikizo la Damu na Sukari, yametajwa kuwatesa wananchi wengi mkoani Kilimanjaro na hivyo wananchi kutakiwa kujijengea utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kujitambua mapema kabla ya tatizo kuwa kubwa.

Rai hiyo imetolewa na mtaalamu wa magonjwa ya kisukari na shinikizo la damu kutoka Hospitali ya Jaffary Polyclinic, Tedy Khumbelle wakati wa kambi ya upimaji afya bure na kuchangia damu katika viwanja vya Mandela mjini Moshi, iliyoandaliwa na Taasisi ya Philemon Ndesamburo Foundation kwa kushirikiana na Moshi FM ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo.

Khumbelle amesema magonjwa ya kisukari na Shinikizo la damu, yameendelea kuwatesa wananchi na wengi hubainika wakati tatizo limekuwa kubwa kwa kuwa hawana utaratibu wa kuchunguza afya.

"Nitoe wito kwa wananchi wajenge utamaduni wa kuchunguza afya zao mara kwa mara maana huwezi kujua tatizo linakuja lini, wasisubiri kuumwa, kwani kuna ambao nimewapima hapa leo wana Sukari na wengine Presha na hawajitambui lakini unakuta sukari iko kwa kiwango cha juu na presha pia iko kiwango cha juu, ni wagonjwa wapya," amesema.

 "Lakini pia nishauri jamii kubadilisha mtindo wa maisha na wafanye mazoezi, kwani siku hizi watu wamatembea na magari muda mrefu na hata watoto wamezoeshwa magari, asubuhi anachukuliwa kupelekwa shule na jioni anarudishwa, hakuna muda wa mazoezi," amesema.


Afisa muhamasishaji wa damu salama kutoka hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Daudi Joho amepongeza hatua hiyo akieleza kuwa mahitaji ya damu ni makubwa ikilinganishwa na ile ambayo wamekuwa wakiipata.

"Mahitaji bado ni makubwa, kwani Hospitali ya KCMC kwa mwaka tunalenga kupata uniti 4,700 ambapo kwa mwezi tunapaswa kupata uniti 392, lakini changamoto ni kwamba hatufikii malengo na uhitaji mkubwa upo kwa kina mama wanaojifungua, watoto chini ya miaka mitano na wale waliopata ajali na upasuaji, lakini jamii bado haina mwamko wa kuchangia damu, tunaendelea kutoa elimu," amesema.

Akizungumza mkurugenzi wa Moshi FM, Lucy Ndesamburo amesema wamekuwa wakifanya shughuli za kijamii na kuweka kambi ya upimaji magonjwa yasiyoambukiza bure kila mwaka, ikiwa ni sehemu ya kumkumbuka Ndesamburo.


 Anasema watu zaidi ya 200 wameweza kujitokeza kupima afya kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari na shinikizo la damu na wengine kuchangia damu ili kusaidia wenye uhitaji.

"Ndesamburo enzi za uhai wake alipenda kusaidia watu wenye uhitaji na michezo hivyo familia tunaendelea kumuenzi kwa kufanya yale aliyokuwa akifanya kwenye jamii na tutaendelea kufanya hivyo kila mwaka tunapokumbuka kifo chake," amesema.

Katika kumbukizi hiyo, mbali na upimaji afya na uchangiaji damu pia kulikuwa na michezo ya aina mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu ulioshirikisha timu mbalimbali za mkoani Kilimanjaro.