Wanaoajiri watoto wakumbushwa kuzingatia sheria

Muktasari:
Akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa kuangalia haki za makundi hayo, mkurugenzi huyo amesema watu wengi wanakiuka sheria za ajira kwa watoto nyumbani hivyo kusababisha wanyanyasike.
Mwanza. Mkurugenzi wa Shirika la utetezi wa haki za watoto, vijana na wanawake (Kiwohede), Justa Mwaituka ameitaka jamii na hasa waajiri wa watoto nyumbani kuzingatia sheria.
Akizungumza kwenye mkutano ulioandaliwa kuangalia haki za makundi hayo, mkurugenzi huyo amesema watu wengi wanakiuka sheria za ajira kwa watoto nyumbani hivyo kusababisha wanyanyasike.
Ameiomba jamii kushirikiana na Kiwohede kupinga unyonywaji na unyanyasaji wa watoto kingono, utumikishwaji nyumbani, ndoa na mimba za utotoni.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Kitivo cha Sheria, Thomas Masanja amesema elimu ndogo na umaskini vinachangia waajiri na jamii kuwatesa watoto.
“Tatizo lipo kwa waajiri kutojua sheria lakini pia umaskini unaoifanya familia ione ni vyema impeleke mtoto kufanya kazi za ndani ili kupata kipato,” amesema Masanja.