Wanaodai kudhalilishwa na meneja watakiwa kurudi shule

Muktasari:

Wazazi wa wanafunzi 25 wa kike wanaosoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Spring Valley mkoani Iringa, wameridhia watoto wao kubaki shuleni baada ya kuhakikishiwa ulinzi na usalama.


Iringa. Wazazi wa wanafunzi 25 wa kike wanaosoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Spring Valley mkoani Iringa, wameridhia watoto wao kubaki shuleni baada ya kuhakikishiwa ulinzi na usalama.

Alfajiri Novemba 12, wanafunzi hao waliandamana hadi Kituo cha Polisi mjini Iringa kulalamikia ukatili wa kingono wanaodai kufanyiwa na meneja wa shule hiyo.

Wanafunzi hao waliwaeleza polisi kuwa walimu na uongozi wa shule yao wameshindwa kuchukua hatua licha ya kuwafikishia malalamiko kila mara.

Baada ya kutoa malalamiko hayo, wanafunzi hao waligoma kurejea shuleni, hatua iliyolifanya Dawati la Jinsia la Polisi na Idara ya Ustawi wa Jamii kuwahifadhi kwa muda katika Shule ya Sekondari Lugalo wakati suala lao likitafutiwa ufumbuzi.

Jana, wazazi wa wanafunzi hao baada ya kujadiliana na dawati la jinsia, uongozi wa shule na ofisi ya ustawi wa jamii, walikubaliana wanafunzi hao warudi shule na kuendelea na masomo yao.

Sambamba na hilo, imefahamika kuwa baada ya meneja huyo kutuhumiwa alikamatwa na polisi na kisha amepewa dhamana.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo alisema dhamana ni kwa mujibu wa sheria, lakini mhusika atafunguliwa mashtaka.

“Wazazi wasiwe na wasiwasi, sheria itachukua mkondo wake,” alisema Moyo, huku akithibitisha kusikia malalamiko kwamba “kuna wanafunzi watatu wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji kingono.”

“Wazazi wasiwe na hofu wakawa na taharuki, sheria itachukua mkondo wake, hiyo ndiyo hali halisi,” alisema Moyo.

Akizungumza katika kikao kilichoshirikisha wazazi, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Iringa, Tiniel Baga alisema baada ya watoto kufika polisi hatua ya kwanza ilikuwa ni kuwaweka kwenye mazingira salama.

“Kwa hiyo tuliwapeleka Lugalo, eneo ambalo ni salama na wale wanaotuhumiwa hawapo wakati tunaendelea na uchunguzi,” alisema Tiniel.

Alisema kwa kuwa hatua za awali zimechukuliwa na wanafunzi wako salama, wanaweza kuendelea na masomo yao.

Ofisa wa Polisi Jamii Wilaya ya Iringa, Violet Siwale alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili sheria ichukue mkondo wake.

Aliutaka uongozi wa shule kabla haujaajiri wafanyakazi, wawe wanawafanyia uchunguzi ili kujiridhisha na maadili yao.

“Jeshi la polisi linaendelea na taratibu za kisheria kwa maana ya kupatikana hati ya jinai,” alisema.

Nguvu Chengula, katibu wa wamiliki wa shule binafsi aliyeongoza kikao hicho aliwashauri wazazi kuamini kuwa watoto wao wapo salama.

Aliwataka wanaoweza kuwachukua watoto wao wafanye hivyo, lakini wahakikishe wanafika shule kila siku.

Simulizi ya watoto

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya watoto walisema walikuwa wakifanyiwa ukatili huo, licha ya kutoa taarifa kwa walimu.

Watoto watatu miongoni mwao wanadaiwa kufanyiwa ukatili huo ikiwamo kupigwa, kupapaswa, kuvuliwa nguo na kupewa dawa za uzazi wa mpango.

“Nilipigwa mpaka alama hizi (anaonyesha mkono), mwalimu alisema nimepasua ndoo lakini sikufanya hivyo,” alisema mmoja wao.

Mwanafunzi mwingine alisema aliitwa ofisini kwa meneja na kulazimishwa kunywa dawa za uzazi wa mpango kama maandalizi ya kufanyiwa ngono.

“Nilipotoka ofisini nikawaambia wenzangu,” alisema mwanafunzi mwingine.

Licha ya malalamiko hayo, Tiniel alisema hakuna mwanafunzi aliyesema ameingiliwa kimwili zaidi ya kupapaswa na kuvuliwa nguo.

Uongozi wawatoa hofu

Katibu Mkuu wa Kanisa la Babtist Tanzania linalomiliki shule hiyo, Mchungaji Alex Bugeraha aliwatoa hofu wazazi, akisema changamoto hizo zinafuatiliwa kwa karibu ili zitatuliwe.

“Sisi kanisa tupo tunaifuatilia kwa karibu na kuhakikisha usalama wao na kila kitu kitaenda sawa na masomo yataendelea kama kawaida,” alisema Bugeraha.