Wanaokata miti ovyo wawaponza wakulima kukosa mvua

Muktasari:

  • Wakazi Mperamumbi walia kijiji chao kugeuka jangwa wakídai chanzo ni baadhi ya wageni kukata miti ovyo kwaajili ya biashara ya mkaa. Watoa ushauri wa Serikali kupata suluhisho.

Kibaha. Vitendo vya ukataji miti kwa ajili ya kutengeneza mkaa vinavyofanywa na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mperamumbi, Kata ya Kwala Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani vimesababisha kukithiri kwa jangwa na kusababisha ukosefu wa mvua hivyo kuongeza ukali wa maisha kwa wananchi waliokuwa wakitegemea kuendesha maisha yao kwa shughuli za kilimo.

Kwa mujibu wa wakazi hao waliokuwa wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi Kijijini hapo Jumatano Machi 22, 2023 wamesema kuwa  hivi sasa hali ya ukame imeendelea kutamalaki kwenye Kijijii hicho hivyo kukwamisha shughuli za kilimo kwani hawapati mvua kikamilifu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma hivyo kutokuwa na uhakika wa chakula.

"Miaka ya nyuma nilikuwa nikilima ekari moja ya mahindi nilikuwa  navuna gunia 10 hadi 8 kwa kuwa mvua zilikuwa zinanyesha kikamilifu lakini hivi sasa hata gunia moja sipati hakuna mvua," amesema Sauda Uliza.

Amesema kuwa wananchi wengi wanajishughulisha kazi ya ukataji mkaa na kuweka kambi porini kísha kuanza kukata miti na kuchoma mkaa.

"Naiomba Serikali ifanye jitihada za kuwaondoa wavamizi hao ili hali ya uoto wa asili irejee tupate mvua tufanye shughuli za kilimo," amesema.

Kwa upande wake, Asha Pendeza amesema kuwa dawa ya kukomesha vitendo vya ukataji miti kwaajili ya mkaa ni Serikali kuwawekea miundombinu wananchi itakayowawezesha kufanya shughuli za kilimo ikiwemo kuwachimbia mabwawa na kuwapa mbegu pamoja na zana za kilimo.

"Serikali waje wakae na wananchi wawape elimu kuhusu kuachana na shughuli za mkaa lakini pia iwawezeshe kwa kuchimba mabwawa ili kilimo cha umwagiliaji kifanyike hali hiyo itapunguza vitendo vya ukataji miti," amesema.

Mjumbe wa Kamati Misitu ya Kitongoji cha Msua, Vumilia Mohamed amesema kuwa hali ya ukame imeendelea kukithiri kwenye Vijiji hivyi na kinachotakiwa ni Serikali kuweka njia mbadala ya kuwawezesha wakata mkaa kuwa na shughuli zingine hasa kuwapa uwezeshaji kwenye kilimo.

Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mpera, Mumbi Franky Kikoti amesema kuwa tangu alipofika kwenye kitongoji hicho miaka mitatu iliyopita amekuwa akishirikiana na watendaji wengine kuhakikisha shughuli za ukataji mkaa zinakoma ingawa bado kuna changamoto zinazojitokeza kwa namna mbalibali.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TFS Kanda ya Mashariki, Methew Ntilicha amesema kuwa katika kukabiliana na vitendo vya ukataji miti kwaajili ya kutengeneza mkaa wamekuwa wakitumia njia mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za kimazingira zinazotikana na vitendo hivyo.

"Nashukuru uongozi wa Mkoa wa Pwani na hata wilaya wote tumekuwa tukishirikiana vizuri kwa nyakati tofauti lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata elimu kwa undani Ili kufuta sheria na kanuni," amesema.

Amesema kuwa Mkuu wa Mkoa huo, Abubakari Kunenge amekuwa akitoa maelekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakifanyiwa kazi na kwamba wanaamini kuwa kadri siku zinavyoenda wananchi wataendelea kubadilika kwa kufuata sheria za misitu.