Wanaouza ardhi kiholela waonywa Wanging'ombe

Muktasari:

  • Kutokana na wananchi wengi kuuza ardhi yao kwa wageni wanaotaka kulima maparachichi, Serikali imewatahadharisha kuhusu uamuzi huo kwani wanaweza kuujutia.

Njombe. Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe, Lauter Kanoni ameonya uuzaji holela wa ardhi unaofanywa na wananchi kwamba wanaweza kujutia uamuzi wao siku za baadaye.

Onyo hilo amelitoa wakati akipokea mifuko 100 ya saruji kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wavulana wenye vipaji maalum inayojengwa katika Kijiji cha Sekalenga wilayani hapa.

Amesema anasikitishwa na kitendo cha wananchi hasa wa Kijiji cha Sekalenga kuuza ardhi kwa raia wa kigeni.

“Mnauza ardhi kwa bei ya chini kwa raia wa Kenya ili waweze kulima maparachichi bila ya kushiriikisha wataalam wa ardhi kutoka halmashauri. Baada ya miaka 10 mtakuja kulia kwani ardhi hiyo mtaikumbuka,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Kanoni amewataka kuacha kuuza ardhi kwani hiyo ndiyo rasilimali yao muhimu hivyo wakiiuza watashindwa kujitafutia maisha hapo baadaye.

Kama wanataka kuuza ardhi hiyo kwa bei ya sasa, amewashauri waende ofisi za halmashauri ili wafanyiwe thamani.

Diwani wa Itulahumba, Thobias Mkane amewataka wananchi wa Kijiji cha Sekalenga kumuunga mkono mkuu wa wilaya kwakuwa amekuwa akijitolea kufanya kazi kwa juhudi kwa masilahi ya wananchi.

"Tangu tumepata wakuu wa wilaya huyu ni baba lao siyo anazungumza tu bali yupo kazini," amesema Thobias.

Meneja wa NHC Mkoa wa Mbeya, Ramadhani Macha amesema lengo la shirika hilo ni kuhakikisha wananchi wanajenga na kuwa na makazi imara kwenye maeneo yao hivyo watashirikiana katika shughuli za maendeleo sambaba na ujenzi shule na zahanati pamoja na taasisi nyingine za Serikali.

"Na hii tumekuwa tukifanya maeneo mbalimbali kutokana na utekelezaji wa shughuli za shirika hilo katika kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii," amesema Macha.