Wanasayansi wagundua sidiria inayobaini saratani ya matiti

Muktasari:
- Wakati wanawake milioni 2.3 waligunduliwa na saratani ya matiti huku 685,000 wakipoteza maisha mwaka 2020, wanasayansi wa nchini Uturuki wamegundua kifaa rahisi na rafiki ‘sidiria’ cha kubaini mapema saratani ya matiti chenye uwezo wa kupima kuzunguka pande zote za titi.
Dar es Salaam. Saratani ya matiti ikiwa ni sababu ya pili ya wanawake kufariki dunia, mwanasayansi wa Kituruki Dk Canan Dagdeviren amegundua kifaa kinachovaliwa kama sidiria kinachoweza kuchanganua matiti yako kutoka pembe nyingi tofauti.
Kifaa hicho kilichowekwa hadharani Oktoba 16 mwaka huu, kinagundulika wakati takribani wanawake milioni 2.3 waligunduliwa na saratani ya matiti huku 685,000 wakipoteza maisha yao mwaka 2020, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Wakati saratani ya matiti inapogunduliwa mapema na ikiwa bado ndani ya eneo moja, inaongeza uwezekano wa kuishi . Iligundulika kuwa katika miaka mitano kiwango cha kupona kilikuwa ni asilimia 99 inasema taasisi ya American Cancer Society.
Dk Canan amesema kifaa hicho kinaweza kusaidia kuongeza viwango vya kuishi kwani kiwango cha kuishi ni asilimia 22 tu kwa wanawake ambao wanagunduliwa katika hatua za baadaye.
Dk Canan na timu yake katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT) Media Lab, wametengeneza teknolojia hiyo, kwa heshima ya shangazi yake ambaye alifariki kutokana na maradhi ya saratani ya matiti.
Kifaa hicho kitawezesha ufuatiliaji wa mara kwa mara wa wagonjwa walioko katika hatari kubwa ya kupata saratani ya matiti kabla ya kufanyiwa vipimo vya uchunguzi wa saratani hiyo vya mara kwa mara vya mammogram.
Mwanasayansi huyo wa vifaa vya MIT amesema alipata wazo hilo wakati amekaa kando ya kitanda cha shangazi yake hospitalini.
Shangazi yake aligunduliwa kuwa na aina ya saratani ya matiti, licha ya kufanyiwa vipimo vya matiti mara kwa mara, na alifariki miezi sita baadaye.
“Ni kifaa rahisi na ambacho kinachoweza kutumika tena na kinaweza kushikamana na sidiria, bila hitaji la mwendeshaji. Skana ndogo ya ultrasound inaweza kutoshea katika moja ya nafasi sita kuchukua picha ya matiti.
“Kuna nafasi sita kwenye kifaa na kamera ndogo ya ultrasound inaweza kuhamishwa kati ya matiti ili uone ndani ya matiti yako kutoka pande zote na kinafanya kazi bila kuhitaji geli ya ultrasound,” amesema Dk Canan.
Amesema inaweza kugundua uvimbe mdogo wa kama sentimita 0.3 na ukubwa wa uvimbe mapema.
Kabla ya kugundulika kwa kifaa hicho, mashine ya Mammogram imekuwa ikitumika kugundua saratani ya matiti ambayo matiti huchunguzwa kwa kipimo cha mionzi, ambapo mionzi hupitishwa kupitia mwili ili kupata picha ya matiti.
Nchini Tanzania wakati saratani ya matiti na shingo ya kizazi zikiongoza, Serikali inakusudia kuandaa mwongozo kwa mwanamke yeyote mwenye umri wa miaka 30 anayekwenda hospitali iwe ni wajibu wa daktari kumuelekeza, kumuelimisha kufanya uchunguzi na kupima.
Mwongozo huo unaandaliwa huku Tanzania ikikadiriwa kuwa na wagonjwa wapya 42,000 kila mwaka na kati yao 4,300 ni wenye saratani ya matiti lakini wanaofika kwenye vituo vya huduma za afya ni 15,900 pekee.
Hayo yamesemwa jana Oktoba 22, 2023 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliposhiriki matembezi ya uelimishaji jamii juu ya saratani, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwezi wa saratani ya matiti ambayo huadhimishwa Oktoba kila mwaka.
“Wizara tunaandaa mwongozo kwa mwanamke yeyote mwenye umri wa miaka 30 anayekwenda hospitali uwe ni wajibu wa daktari kumwelimisha kufanya uchunguzi mwenyewe wa saratani ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi, tukiwagundua mapema matibabu yatakiwa rahisi badala ya kupita kwenye mizunguko ya tiba za kemikali na mashine za mionzi,” amesema Waziri Ummy.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2017, vifo vitokanavyo na saratani ya matiti vinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2030, huku idadi ya wagonjwa wapya ikitarajiwa kuongezeka kwa asilimia 82.