Wanasiasa waibuka upya mitandaoni

Wednesday April 07 2021
wanasiasapic
By Daniel Mjema

Moshi. Nini kimetokea? hili ndio swali Watanzania wengi wanajiuliza baada ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuonekana kama wamebadili gia angani na wengine hususan wabunge, wakitumia mitandao ya kijamii kutoa hisia zao.

Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala ndiye amekuwa gumzo zaidi mitandaoni kuanzia juzi baada ya kubadili msimamo wake wa awali kuhusiana na ugonjwa wa Covid-19.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaona kuna sababu zinazosababisha hali hiyo, mojawapo ni uwepo wa wanaotaka kutembea na mwendo wa Rais Samia Suluhu Hassan na pili wako ambao ni bendera fuata upepo wanaotafuta fursa.

Lakini, wachambuzi hao wanaona wako ambao walishindwa kuonyesha misimamo yao kutokana na aina ya uongozi uliokuwepo, lakini kwa sasa ni kama wametoka kifungoni, hivyo wanataka kuonyesha sura zao halisi kwa Rais Samia. Ukiacha Dk Kigwangala, wengine waliogeuka gumzo mitandaoni ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba ambao jumbe zao kupitia kurasa zao za Twitter zimekuwa na ujumbe wa mafumbo zaidi.

Wengine ni Mbunge wa Arusha mjini, Mrisho Gambo na mawaziri wa zamani katika Serikali ya awamu ya nne, Balozi Khamis Kagasheki aliyepata kuwa Mbunge wa Bukoba mjini na Profesa Mark Mwandosya.

Dk Kigwangala amekuwa gumzo zaidi kutokana na kubadili msimamo wake hasa katika suala la ugonjwa wa corona, ambako huko nyuma alionyesha kutilia shaka matumizi ya chanjo na akawa msitari wa mbele kuhamasisha kujifukizia.

Advertisement

Lakini juzi katika mahojiano na Radio moja na baadae jumbe zake katika akaunti wake ya Twitter, Dk Kigwangala ametaka Serikali irudi katika sayansi katika kupambana na corona na akienda mbali zaidi akipigia chapuo matumizi ya chanjo. Dk Kigwangala alipendekeza mtambo wa kupiga nyungu uliopo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Jijini Dar, es Salaam uvunjwe na njia nyingine za kitaalamu za kupambana na Covid-19 ikiwamo kufanya tafiti za kisayansi.

Msimamo wake huo mpya umepata upinzani, huku baadhi ya wachangiaji katika mitandao ya kijamii wakimuona kama ni mtu asiye na msimamo, kwani ushauri huo alipaswa kuutoa wakati akiwa ndani ya Baraza la mawaziri.

Jumbe ambazo zimeendelea kufikirisha ni ya Nape aliyeandika. “Maisha mazuri ukiwa na furaha, lakini maisha ni mazuri zaidi na yana maana zaidi kama kuishi kwako kuna wafanya watu wengine pia wafurahi. Nawatakia pasaka njema.”

Makamba naye aliandika simulizi ndefu ya dereva wa Ikulu aliyetofautiana naye na mwisho akaandika “Leo ni Pasaka. Yesu alifariki msalabani ili tusamehewe dhambi zetu. Pasaka ni wakati wa kusamehe. Tusameheane.

Balozi Kagasheki alizungumzia suala la Rais Samia kuikemea Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutowafilisi wafanyabiashara. Suala ambalo pia Gambo, aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha alilizungumzia.

Advertisement