Wanaume walio hatarini kupata saratani ya tezi dume

Wanaume walio hatarini kupata saratani ya tezi dume

Muktasari:

  • Vinasaba, ulaji wa nyama nyekundu na unene ni mojawapo ya visababishi vikuu vya ugonjwa na saratani ya tezi dume kwa wanaume.


Vinasaba, ulaji wa nyama nyekundu na unene ni mojawapo ya visababishi vikuu vya ugonjwa na saratani ya tezi dume kwa wanaume.

Kutokana na tatizo hilo, wataalamu wa afya wanashauri wanaume wenye vinasaba vya ugonjwa huo kuwahi hospitali, huku wengine wakitakiwa kuzingatia mlo sahihi hasa kuepuka ulaji wa nyama nyekundu.

Akizungumza na Jarida la Afya, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga ya Saratani kutoka Taasisi ya Ocean Road, Dk Crispin Andrew anasema kuna aina zaidi ya 200 za saratani na saratani ya tezi dume inaathiri wanaume wenye umri kuanzia miaka 50.

Anasema saratani ya tezi dume ndio ugonjwa unaoongoza kwa vifo vya wanaume, huku ikiwa nafasi ya nne katika orodha ya zaidi ya saratani 200.

Anasema kwa mujibu wa tafiti, watu weusi wapo katika hatari mara mbili zaidi ya kuugua ugonjwa huo kuliko watu weupe.

“Sababu za kuugua inawezekana ikawa umri, unene, kingine ni vinasaba kwa sababu inaonekana watu weusi ni familia moja, lakini pia mfumo wa ulaji wa vyakula, ikiwemo matumizi ya nyama nyekundu nao unachangia,” anasema Dk Kahesa.

“Pamoja na kuwa umri ni chanzo pia na hauwezi kuzuilika, lakini jambo la msingi ni kubadilisha mwenendo wa maisha, hususan katika vyakula, inatakiwa kula matunda, mboga za majani na kuachana na nyama nyekundu,” anasema Dk Kahesa.

Kuhusu dalili, Dk Kahesa anasema mwanzoni hauna dalili na kwamba wengi wanaokwenda hospitali wanakuwa na shida kwenye haja ndogo, maumivu ya mifupa na kukosa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.

Anasema saratani ya tezi dume inaweza kusambaa kwenda kwenye viungo vingine, huku wengine wanaweza wasipone kabisa, bali kutuliza tu.

Anafafanua saratani ya tezi dume ipo katika hatua nne ambazo ni uvimbe mdogo kwenye kokwa, uvimbe hadi nje ya kokwa, kusambaa kwenye viungo vingine na hatua ya nne ni kusambaa kwenye viungo vya mwili mzima, huku akitolea mfano uti wa mgongo.

Daktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Deogratius Mahenda anasema tezi dume katika hali ya kawaida si ugonjwa, bali ni kiungo ambacho kipo katika mwili wa mwanamume.

Anasema kazi yake kubwa hasa wakati wa kujamiiana hutoa majimaji yanayochanganyikana na mbegu za kiume, ili ziende sehemu ya uzazi ya mwanamke na kutengeneza ujauzito.

Anafafanua kadri mwanamume anavyokua, ukubwa wa tezi unabaki kati ya gramu 15 hadi 20 au 25, na hiyo ni kwa sababu mwili unatengeneza chembe hai kila siku, lakini chembe hai ambazo zimefika ukomo zinakufa.

“Kwa hiyo unakuta kwamba ukubwa wa tezi unabaki palepale, mabadiliko yanakuja kutokea kwa baadhi ya wanaume wakiwa na miaka 40, wengine miaka 50.

“Kuanzia hapo ndipo mabadiliko yanaanza kutokea, ule mfumo uliokuwepo wa kudhibiti ukubwa wa tezi unakwisha au unapungua kufanya kazi yake, kwa hiyo zile chembe hai zinazotengenezwa zinazidi kufanya tezi lizidi ukubwa, ule mfumo wa kuziondoa zile ambazo zimefika ukomo wa kuishi unakuwa haupo, kwa hiyo sababu ya kwanza ni umri,” anasema.

Dk Mahenda anaeleza kuwa, mabadiliko hayo yanafanya tezi kuwa kubwa zaidi ya kawaida, hivyo kubana njia ya mkojo, pia vitu ambavyo vinaweza kupelekea mtu kuwa na mabadiliko hayo kwa mapema zaidi ni wale ambao walipata maambukizi ya magonjwa ya kujamiiana kama kisonono na UTI.

Anasema hivyo vinaweza vikachochea tezi kukua kwa haraka katika umri mdogo, na kama kuna vinasaba katika familia pia vinachangia.

Dalili

Anasema moja ya dalili za ugonjwa huo ni mabadiliko ya utoaji haja ndogo, atachukua muda kidogo kuanzisha kuutoa na wengine hulazimika kutumia nguvu za misuli ya tumbo ili kusukuma mkojo utoke.

“Mtu mwenye ugonjwa huu anapopata haja ndogo inakuwa inakatika katika na mwishoni utamalizika kwa matone matone yasiyokatika kwa muda mfupi. Na atahisi kibofu bado hakijaisha mkojo, baada ya muda mfupi tena atahisi kwenda kutoa haja.

“Mwingine akihisi mkojo anashindwa kuudhibiti kabla hajafika maliwatoni unamtoka na anachafua nguo,” anasema na kuongeza wengine usiku hupata haja mara nyingi kuliko kawaida yake.

Anashauri mtu anapoona dalili kama hizo ni vizuri awahi kituo cha afya kupata matibabu.