Wanawake Chadema walikumbusha Jeshi la Polisi mauaji raia mahabusu
Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Catherine Ruge
Moshi. Katibu wa Baraza la wanawake Chadema (Bawacha) Catherine Ruge amesema hawafurahishwi na vitendo vya mauaji yanayotokea maeneo mbalimbali nchini, ambayo yanafanywa na Jeshi la Polisi hasa katika vituo vya polisi na maeneo mengine ya ukamataji.
Ruge ameyasema hayo jana Machi 8, 2023 wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyoandaliwa na baraza hilo na kufanyika kitaifa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
"Hatufurahishwi na mauaji yanayotokea maeneo mbalimbali nchini, yanayofanywa na jeshi la polisi, hasa katika vituo vya polisi na maeneo mengine ya ukamataji," amesema.
"Bawacha tunaendelea kutetea haki ya kuishi, haki ya uchaguzi, haki ya kupata ajira, haki ya kuoata huduma bora za afya hasa wanawake na watoto, haki hizi zote zimekuwa zikivunjwa kinyume cha katiba, hiki ndicho kiini cha mapambano yetu kama Bawacha," amesema.
Aidha Ruge ameshauri kuboreshwa kwa mitaala ya elimu ili kuwezesha wanafunzi kujifunza taaluma kwa kuzingatia mahitaji ya wakati uliopo, ikiwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza mpango mahususi wa kuwezesha mitaji na miundombinu wanafunzi wa kike wanaosoma masomo ya sayansi na teknolojia ili kuwa na kizazi endelevu katika sekta hiyo.
Amesema vifo vya kina mama wanaojifungua na watoto bado viko juu na teknolojia na ubunifu bado havijaokoa maisha ya mama mjamzito na mtoto mchanga katika Taifa na hivyo kutoa wito kwa Serikali kuweka utaratibu wa kutenga fedha kwa ajili ya masuala ya utafiti kwa kutumia teknolojia na ubunifu ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa za kidigitali na kusaidia kuokoa afya ya mama na mtoto.
"Wakati tunazungumza kuhusu umuhimu wa teknolojia katika kujikwamua, wanawake Tanzania wanalima kwa kutumia jembe la mkono, ni wakati sahihi sasa kwa Serikali kuwekeza katika kuwezesha wanawake kupata mitaji ya pembejeo ili kuweza kulima kilimo cha kisasa na chenye tija," amesema.
Amesema, "Mifumo rasmi ya kiuchumi na fedha na kiuchumi haijumuishi wanawake wengi wa kitanzania hasa wanaoishi vijijini, mathalani taasisi za kifedha kama benki haziwapi fursa za kupata mitaji wanawake hawa. Hata hivyo miaka mitano iliyopita ujumuishaji wa wanawake katika fedha kwa njia ya kidigitali uliongezeka, lakini baada ya kuweka tozo katika miamala ya simu, imepunguza ujumuishaji huo na kuathiri uchumi wa wanawake," amesema.