Wanawake JWTZ Land Force watoa mbinu kukomesha ukatili wa familia

Wanawake kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Land Force,  Msangani Kibaha, Mkoa wa Pwani wakiwa katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Bagamoyo kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani.

Muktasari:

  • Ujasiriamali na taaluma mbalibali kwa wanawake  ndiyo dawa dhidi ya vitendo vya ukatili kwao na familia kwa ujumla.

Bagamoyo. Iwapo wanawake watajikita kwenye shughuli za ujasilimali na kujiendeleza kitaaluma kutasaidia kupunguza vitendo vya ukatili dhidi yao kutoka kwa wanaume wenye silika hiyo na hatimaye kujenga jamii bora.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Machi 8, 2023 na wanawake kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Land Force,  Msangani Kibaha, Mkoa wa Pwani wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Bagamoyo kwa ngazi ya Mkoa wa Pwani.

"Mwanamke ni kiunganishi kikuu ndani ya familia, hivyo hatakiwi kuyumba katika nyanja za kiuchumi na kielimu na hata malezi akiyumba atakuwa ameyumbisha familia na jamii," amesema Meja Glory Mamuya.

Amesema kuwa hata akiwa mwajiriwa kwenye taasisi ya umma au hata binafsi suala la ujasiriamali hatakiwi kulikwepa kulingana na uchumi wa sasa kwani bila kufanya hivyo atakuwa anajirudisha nyuma.

Kwa upande wake Ruteni Sikujua Shamte amesema kuwa wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake kwenye mataifa mbalimbali wanawake wanapaswa kuendeleza ujasiri wao wa kupambana na vitendo vya ukatili vinavyochangia kurudisha nyuma maendeleo.

Naye Staff Sajenti Maria Pankras ameitaka jamii kutorudi nyuma katika kushirikiana na Serikali kupambana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili kujenga Taifa bora na imara.

Kwa upande wake, Jane Gogi amewataka wanawake kujiunga kwenye vikundi mbalimbali vya ujasiriamali.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshwaji Kiuchumi Wanawake Mkoa wa Pwani, Mariam Ulega amesema kuwa jitihada zinazofanywa na mkoa huo katika kuwakwamua kiuchumi wanawake ni pamoja na kuwapa elimu ya ujasiriamali pamoja na mikopo kutoka halmshauri na taasisi za fedha.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Pwani, Zainabu Vullu amesema kuwa dunia kwa sasa iko kwenye wakati mgumu na hii inatokana na baadhi ya watu kuacha maadili mema na kujiingiza kwenye vitendo  viovu jambo ambalo linapaswa kupigwa vita na kila mmoja.

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Okash amewataka wanawake wenye dhamana mbalimbali mkoani humo kuzitumia vizuri ili kulinda jamii katika nyanja mbalimbali.