Wanawake Serengeti wapewa simu janja

Mkurugenzi wa Shirika la Hope For Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwel. Picha na Anthony Mayunga

Muktasari:

  • Shirika la Hope For Girls and Women Tanzania lenye makao makuu yake Wilaya ya Serengeti limetoa simu janja 87 kwa wanawake kuwawezesha kupata elimu ya masoko na shughuli mbalimbali.

Serengeti. Shirika la Hope For Girls and Women Tanzania lenye makao makuu yake Wilaya ya Serengeti limetoa simu janja 87 kwa wanawake kuwawezesha kupata elimu ya masoko na shughuli mbalimbali.

Mkurugenzi wa shirika hilo,  Rhobi Samwel  leo Jumatatu Machi 8, 2021  ameieleza Mwananchi Digital kuwa lengo ni kuvunja daraja la wanaume kuonekana ndio wanamiliki mifumo ya taarifa sahihi vijijini kuhusu mambo ya kiuchumi.

"Tunapoadhimisha siku ya mwanamke duniani tunaangalia tulipotoka, tulipo na tunapokwenda  hivyo kuwapa simu janga wanawake hasa wajasiriamali ni kuwaunganisha kwenye ulimwengu wa kisasa ambao mtu anapata maarifa na masoko kupitia mitandao," amesema.

Amesema pia wanazitumia kutoa taarifa za matukio ya ukatili kwa watoto hasa wa kike na zimesaidia kuleta mabadiliko makubwa kwa kuwa taarifa zinafika na hatua kuchukuliwa kwa haraka kuwasaidia wanaokuwa wametendewa.

"Mwanamke anapopewa jukumu anawajibika vizuri  zaidi, hivyo sisi maadhimisho haya tunayatumia kama sehemu ya tathmini kama kuna mabadiliko kwa wanawake hasa katika kujitambua kisiasa, kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi kwa watoto," amesema.

Rhobi ni mhanga wa ukatili wa kijinsia kwa kuwa alikatishwa masomo na kuozwa lakini  hakukata tamaa alipambana hadi kufikia ndoto ya kuongoza shirika linalosaidia watoto na wanawake wanaofanyiwa ukatili wa ukeketaji, ndoa za utotoni na vipigo katika wilaya za Serengeti na Butiama.