Wanawake, vijana wapewa vifaa vya Sh3.5 milioni

Mbunge wa Viti Maalum ( CCM) Mkoa wa Mara  (wanne kulia)  Agnes Marwa akiangalia baadhi ya bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa na moja ya vikundi vya wanawake katika kata ya Iringo Manispaa ya Musoma . Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Vikundi vya wanawake na vijana Kata ya Iringo mkoani Mara vimepewa msaada wa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Sh3.5 milioni na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) mkoani humo, Agnes Marwa ili kuboresha shughuli zao za ujasiriamali.

Musoma. Vikundi saba vya wanawake na vijana katika Kata ya Iringo Manispaa ya Musoma vimepewa msaada wa vifaa vya Sh3.5 milioni vitakavyotumika kwenye shughuli zao za ujasiriamali.

Vifaa hivyo vikiwemo viti, majiko ya gesi,miamvuli, majembe na makoleo vimetolewa leo Jumatano Septemba 20, 2023 na Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Mara, Agnes Marwa. 

Akizungumza na vikundi hivyo, Agnes amewataka wanawake kujiunga na vikundi vya kijasiriamali ili kupewa mikopo inayotolewa na Serikali ili kuepuka madhara yatokanayo na mikopo umiza.

“Mikopo umiza pia ni mojwapo ya  chanzo cha migogoro  kwenye ndoa kwani mwanamke unapokuwa na mkopo huo unakuwa hauna amani na mwisho wa siku unashindwa  kusimamia malezi ya familia kama mama maana muda wote unawaza  marejesho yake,”amesema 

Amesema njia pekee ya wanawake kuondokana na mikopo hiyo ni kujiunga na vikundi kama ambavyo Serikali imeelekeza ili waweze kutumia fursa za mikopo isiyodhalilisha utu wao.

“Kwa kushirikiana na UWT (Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi) mkoa, nitahakikisha nazifikia kata zote za Mkoa wa Mara kuwaunga mkono wanawake waliopo katika vikundi. Hatutaki wanawake wakimbie familia zao na kudhalilika kisa tu  marejesho ya kausha damu,”amesema 

Mbali na vifaa hivyo, mbunge huyo pia ametoa msaada wa jezi seti mbili na mipira minne kwa timu mbili za mpira wa miguu katika kata hiyo ili kuimarisha sekta ya michezo na mahusiano mema baina ya vijana.

Naye Mjumbe wa Taifa wa Baraza Kuu UWT, Mgore Miraji amewaasa wanawake kuchukua mikopo kulingana na biashara zao ili waweze kumudu marejesho.

“Serikali inatengeneza mazingira sasa na sisi wanawake hebu tuchukue mikopo kulingana na biashara tulizonazo na hii itasaidia kuwa na nidhamu ya pesa na kuepuka matumizi yasiyokuwa rasmi kisha kuinua biashara zetu na kuwa kubwa zaidi,”amesema Mgore

Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mtanda amesema Serikali imedhamiria kuwaimarisha kiuchumi wanawake nchini kutokana na umuhimu wao katika jamii.

“Ule usemi kuwa adui wa mwanamke ni mwanamke mwenyewe hivi sasa hauna nafasi, endeleeni kushirikiana,kupendana na kuaminiana ili kuipa Serikali nafasi nzuri ya kuwatengenezea mazingira mazuri zaidi ya kuimarika kiuchumi,”amesema Mtanda