Wanawake wahimizwa kusoma sayansi

Muktasari:

  • Katika kuongeza idadi ya wahandisi wanawake nchini, wanafunzi wa kike nchini wamehimizwa kusoma masomo ya sayansi yatakayowawezesha kuwa wataalamu kwenye taaluma hizo.

Dar es Salaam. Katika kuongeza idadi ya wahandisi wanawake nchini, wanafunzi wa kike nchini wamehimizwa kusoma masomo ya sayansi yatakayowawezesha kuwa wataalamu kwenye taaluma hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Rais wa Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET), Mhandisi Gemma Modu amesema hadi sasa bado idadi ya wahandisi haswa wanawake hairidhishi.

Dk Gemma amesema hadi sasa wahandisi waliosajiliwa ni takribani 35, 0000 huku kati ya hao wanawake ni 4000 pekee.

Hivyo amesema moja katika ajenda watakayoijadili katika mkutano wa wahandisi unatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam moja ya ajenda watakaozizungumza ni pamoja na kuangalia namna gani watashirikiana kwa pamoja na jamii katika kuhamasisha wanafunzi kusoma fani ya uhandisi.

Amesema  mkutano huo ambao ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhandisi duniani ambao umeandaliwa na IET utahudhuriwa na washiriki wapatao 200 kutoka taasisi za umma na binafsi.

“Wote tumeshuhudia miaka ya hivi karibuni kushuka kwa ufaulu wa masomo ya sayansi hivyo wahandisi ikiwa ni sehemu ya jamii ina wajibu wa kushiriki katika jitihada za pamoja ili kuokoa hali hiyo”

Pia amesema mkutano huo unaongozwa na kauli mbiu isemayo ' Ubunifu wa Uhandisi kwa Ulimwengu Unaostahimili Zaidi kwa kuzingatia kuwa dunia kwa sasa inapitia katika maendeleo makubwa ya Sayansi na Teknolojia.

"Kauli mbiu hiyo inaendana na mazingira ya sasa kwani tunaishi kwenye uchumi na jamii zinazoendeshwa na nguvu ya teknolojia ambayo maendeleo yake ni makubwa yanayochochewa zaidi na mapinduzi ya kidigitali yanayoambatana na ubunifu" alisema.

Hivyo amesema kupitia mkutano huo taasisi zitakazoshiriki zitapatiwa fursa ya kuonyesha ubunifu waob katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea nchini pamoja na kazi zinazohusisha fani ya uhandisi.

Tangu mwaka 2019 kila ifikapo Machi 4 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya wahandisi duniani ambayo hutoa fursa ya kutambua na kuthamini mchango wa wahandisi katika kuleta maendeleo