Wanawake wanaofanyiwa ukatili, udhalilishaji mitandaoni wapewa mbinu

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben.

Muktasari:

  • Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimewataka wanawake wanaopitia changamoto ya ukatili na udhalilishaji mitandaoni kutoa taarifa katika vyombo vya usalama ili waweze kusaidiwa na kulindwa dhidi ya ukatili huo kabla ya kupatwa na madhara makubwa.

Dar es Salaam. Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kimewapa ushauri wanawake wanaopitia changamoto ya ukatili na udhalilishaji mitandaoni kutoa taarifa katika vyombo vya usalama ili waweze kusaidiwa na kulindwa dhidi ya ukatili huo kabla ya kupatwa na madhara makubwa.

Pia kutoa wito kwa wanawake kutumia vyema teknolojia ikiwemo mitandao ya kijamii kuibua changamoto zinazowakabili wanawake na watoto wa kike, kuhamasisha kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, na kuwapongeza wanawake na watoto wa kike, waliofanya vyema katika jamii yetu.

Wito huo umetolewa Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Rose Reuben kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka.

Kwa mwaka huu, siku hii inaadhimishwa ikipambwa na kaulimbiu isemayo, Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia: Chachu Katika Kuleta Usawa wa Kijinsia.

Katika taarifa aliyoitoa Rose leo Machi 8, 2023 inaeleza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanatoa nafasi ya kutafakari, hatua madhubuti za siku zijazo zitakazowezesha matumizi sahihi ya kidijitali kwa watoto wa kike.

Hebu fikiria dunia yenye usawa wa kijinsia, isiyo na upendeleo wala unyanyasaji wa kijinsia, dunia jumuishi isiyokuwa na habari potofu, ni muhimu tuungane kwa pamoja kujenga usawa kwa kuongeza ubunifu na matumizi chanya ya teknolojia kwa wanawake na watoto wa kikeĀ 

Taarifa hiyo pia inaeleza kuwa utafiti uliofanywa na taasisi ya Women at Web kwa kushirikiana na TAMWA, umebainiĀ  asilimia 79 ya wanawake wanasiasa na wanaharakati wa kisiasa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020.

"Ni dhahiri kuwa teknolojia imeleta neema lakini wakati mwingine, inatumiwa vibaya na kusababisha madhara kwa makundi mbalimbali hasa wanawake," amesema.

Hivyo inatoa wito kwa jamii kujikita katika matumizi sahihi ya teknolojia zilizopo na kuzitumia vyema fursa zinazopatikana pamoja na kuchagiza ubunifu na maendeleo kwa mlengo wa usawa wa kijinsia.

"Tunaamini katika nguvu chanya ya teknolojia na tunatamani wanawake na wasichana waitumie kwa ubunifu ili waweze kujikomboa kijamii, kiuchuni na kisiasa," amesema.