Wanne kortini kwa kukutwa na madini bila kibali

Muktasari:

  • Wafanyabiashara wanne  wakiwemo raia watatu wa Sri-Lanka wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kukutwa na madini bila kuwa na kibali na kuisababishia Serikali hasara ya Sh42.9 milioni.

 Dar es Salaam. Wafanyabiashara wanne  wakiwemo raia watatu wa Sri-Lanka wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kukutwa na madini bila kuwa na kibali na kuisababishia Serikali hasara ya Sh42.9 milioni.

Washtakiwa hao ni Mohamed Hashim (47), Mohamed Muwas (26), Mohamed Yoonus (28) wote raia wa Sri-Lanka na wakazi wa Ilala na Mehboob Rattansi (62) ambaye ni rais wa Tanzania mkazi wa Msasani.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao leo Alhamisi Januari 14, 2021 na wakili wa Serikali mwandamizi, Wankyo Simon mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, Godfrey Isaya.

Wakili Simon amedai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwamba Januari 8, 2021 jijini Dar es Salaam walitenda kosa la kuongoza genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Shtaka la pili, siku na maeneo hayo washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa  walikutwa wakimiliki aina 43 za madini ghafi yakiwemo ya rubi na  Tanzanite yenye uzito wa gramu 2,054.4 ya Sh25,788,353  bila kuwa na kibali kutoka kwa kamishna wa madini.

Wakili Simon amedai katika shtaka la tatu ambalo ni kukutwa na madini yaliyoongezewa thamani yenye  uzito wa  na Carat 85.89 ya Sh17,132,702  bila kibali.

Mashtaka mengine ni kununua madini bila leseni, kuisababishia hasara Serikali na kutakatisha Sh 42.9 milioni kwa kujihusisha katika miamala ya fedha zinazotokana na madini hayo wakati wakijua pesa hizo ni zao la kosa la kumiliki madini bila kuwa na kibali.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka, Isaya aliwataka kutojibu chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

Hakimu huyo amesema shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Isaya ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 28, 2021 itakapotajwa na washtakiwa walirudishwa rumande.