Waomba mashimo ya mchanga yafukiwe

  • Baadhi ya mashimo yaliyopo kwenye kata za Muungano ,Bondeni na Bomang'ombe wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Wananchi wa kata za Muungano, Bomang'ombe na Bondeni zilizopo Mamlaka ya mji mdogo wa Bomang'ombe wilayani Hai wameomba Halmashauri hiyo kuyafukia mashimo yaliyotokana na uchimbaji mchanga yafukiwe kwa usalama wao.

Hai. Baadhi ya wananchi wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro wameiomba Halmashauri hiyo kuyafukia mashimo yanayotokana na kuchimbwa mchanga kwa ajili ya ujenzi ili kuweka mji katika mazingira mazuri.

Wananchi hao kutoka kata za Muungano, Bomang'ombe na Bondeni zilizopo Mamlaka ya mji mdogo wa Bomang'ombe wameomba Halmashauri hiyo kuyafukia mashimo hayo kabla hayajaleta hatari kwa Wananchi.

"Kwa kweli mashimo ni mengi kwenye hizi kata za Mamlaka ya mji mdogo wa Bomang'ombe na yalitokana na uchimbwa mchanga kwa ajili ya ujenzi kabla mji haujakuwa mkubwa. Tunaomba yafukiwe kabla hayajaleta athari kwa wananchi,” amesema Anna Shirima mkazi wa mtaa wa Kingereka.

Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Kingereka A, Habibu Lema, amesema kwenye mtaa wake yapo mashimo matano makubwa ambayo ni hatari kwa wananchi hasa watoto wadogo wanaocheza katika maeneo hayo.

Ambapo mashimo haya yamekuwa yakiuweka mji katika mazingira mabaya kwani yapo kwenye makazi ya watu na pia kuwa hatarishi kwa wananchi na wanyama wanaopita katika maeneo hayo kungukia kwenye mashimo

Hivi karibuni Diwani wa Kata ya Bondeni Vicent Songoi aliitaka Halmashauri hiyo kufukia mashimo yaliyopo kwenye kata tatu zilizopo chini ya mamlaka ya mji mdogo wa Bomang'ombe na kata jirani ikiwamo ya Masama Kusini.

Akizungumzia kero hiyo, Mkurungenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dionis Myinga amesema atalifanyia kazi Jambo hilo ili kupunguza athiri iliyoweza kujitokeza

"Ni kweli kwamba mashimo haya ni hatarishi, iwe kwa wanadamu au wanyama. Sisi na Wataalamu wetu tutapita kote kuainisha haya mashimo, halafu tutafanya jitihada ya kuhakikisha kwamba tunayafukia kwa pamoja,” amesema Myinga