Wapendekeza taulo za kike ziondolewe kodi

Muktasari:

  • Wadau wamependekeza iwepo mikakati ya muda mrefu kuhakikisha taulo za kike zinapatikana bure kwa wanafunzi ili wabaki shule na kupunguza mdondoko kwa watoto wa kike katika elimu.

Dar es Salaam. Wadau wamependekeza iwepo mikakati ya muda mrefu kuhakikisha taulo za kike zinapatikana bure kwa wanafunzi ili wabaki shule na kupunguza mdondoko kwa watoto wa kike katika elimu.

Bajeti ya mwaka 2018/2019 Serikali ilipunguza gharama hizo, mwaka mmoja baada ya kutolewa kwa kodi, Serikali iliirudisha tena kwa madai kuwa wafanyabiashara hawajapunguza bei kama ilivyokusudiwa.

Hata hivyo, matarajio ya wadau wengi, mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22 yaliyowasilishwa bungeni juzi na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba yangekuja na suluhisho.

Mdau wa hedhi mashuleni, Hyasintha Ntuyeko alisema kama ambavyo Serikali imeondoa kodi za taulo za mikojo za watoto ingefanya hivyo hivyo kwenye taulo za hedhi.

“Ili kumpunguzia msichana na mwanamke changamoto mbalimbali anazozipitia wakati wa hedhi hili ni jambo lililotazamiwa na wengi. Malighafi zinazotumika kutengenezea taulo za kike na taulo za mikojo za watoto ni zilezile, binafsi sioni kwa nini hawakutoa kodi kwenye taulo za hedhi pia,” alisema Hyasintha, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kasole Secrets.

Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi alisema bidhaa ya taulo haikutakiwa hata kuuzwa, hasa kwa wanafunzi kwa kuwa ni muhimu na wanawake hawachagui kupata hedhi, hivyo kutozwa kodi kwa kupata hedhi kila mwezi si jambo la kibinadamu.

Gyumi alisema kodi iliyoshushwa mwaka 2019 katika viwanda kutoka asilimia 30 kwenda 25 bado haisaidii.

“Tunahitaji misamaha yote ili kupata unafuu mkubwa zaidi. Ingawa kodi katika uzalishaji imeshushwa kwa asilimia tano ilimradi kodi ya ongezeko la thamani (VAT 18%) bado itakuwepo, mlaji wa mwisho hatapata unafuu.

Utafiti uliofanywa na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef), ulionyesha wasichana hukosa masomo siku nne hadi tano kwa mwezi kutokana na hedhi.

Utafiti huo ulionyesha msichana mmoja kati ya kumi huacha shule kila mwaka kutokana na kukosa vifaa vya kujihifadhi wakati wa hedhi.

Mbunge wa Jimbo la Momba, Condester Sichwale alisema kilichowasilishwa juzi ni mapendekezo ya bajeti kutokana na namna wizara mbalimbali zilivyowasilisha vipaumbele katika bajeti zao.

Alisema wanafanya mapitio hivyo nafasi ya kuboresha ipo.