Wapigana mishale wakigombea mpaka, sita wajeruhiwa
Muktasari:
Watu sita wamejeruhiwa kwa kuchomwa mishale baada ya kuibuka ugomvi uliosababishwa na mggoro wa ardhi katika vijiji vya Remung'oroli wilayani Serengeti na Mikomariro wilayani Bunda Mkoa wa Mara.
Musoma. Watu sita wamejeruhiwa kwa kuchomwa mishale sehemu mbalimbali za miili yao huku nyumba nne zikibomolewa baada ya kutokea vurugu kati ya wakazi wa kijiji cha Remung'oroli Wilaya ya Serengeti na wakazi wa kijiji cha Mikomariro Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Chanzo cha vurugu hizo kinaelezwa kuwa ni ugomvi wa mpaka kati ya ya vijiji hivyo tatizo lilolodumu zaidi ya miaka 20.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salim Morcase amesema vurugu hizo zilitokea Septemba 17, 2023 saa 10:30 jioni baada ya watu kutoka kijiji Cha Mikomariro kwenda kuchunga kwenye eneo lenye mgogoro maarufu kama Kisambusa.
"Baada ya kufika pale Kisambusa wenzao kutoka Remung'orori walikuja ndipo wakaanza kupigana kwa kurushiana mishale na kupelekea watu watano kutoka kijiji cha Mikomariro kujeruhiwa huku mtu mmoja kutoka kijiji cha Remung'oroli naye akijeruhiwa,"amesema
Amewataja majeruhi ni Mkami Itogoro aliyejeruhiwa mguu wa kulia, Nyamuhanga Wambura aliyejeruhiwa mkono wa kushoto, Juma Werema aliyejeruhiwa mguu wa kulia, Mang'era Wambura aliyejeruhiwa shingoni na Isore Mtegetu aliyejeruhiwa kwa mshale tumboni wote wakazi wa Mikomariro huku Mataiga Mwita wa kijiji cha Remung'oroli akijeruhiwa kwa mshale shingoni.
"Watu wote sita walipatiwa matibabu na kisha watano kuruhusiwa kuondoka isipokuwa Isore Mtegetu (28) mkazi wa Mikomariro aliyejeruhiwa kwa mshale tumboni bado amelazwa katika Kituo cha Afya Mugeta kwaajili ya matibabu zaidi,"amesema
Amesema nyumba nne zilizobomolewa ni za wakazi wa kijiji cha Remung'oroli na kwamba baada ya kutokea tukuo hilo jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na kuweza kurejesha hali ya amani.
Kamanda Morcase amesema hivi sasa suala hilo linashughulikiwa kiutawala ili kuweza kupata suluhisho la kudumu na kwamba jeshi la polisi bado lipo eneo la tukio kwaajili ya kuimarisha usalama.