Wapinzani walia kuvunjwa kwa kamati za Laac, Pac sakata la CAG

Mbunge wa Kibamba John Mnyika (Chadema)  akizungumza kuhusu wajumbe wa kamati mbili za bunge LAC na PAC kubadirishwa. Kulia ni Aly Saleh na kushoto ni Nagenjwa  Kaboyoka

Muktasari:

Wabunge wa upinzani wameelezea kusikitishwa na uamuzi wa Spika Job Nduga kuzivunja kamati za Laac na Pac, wataka zirejeshwe haraka wakitishia kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Spika

Dodoma. Kambi ya upinzani bungeni imemtaka Spika wa Bunge, Job Ndugai kubadili uamuzi wa kuwahamisha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), vinginevyo watawasilisha hoja kutokuwa na imani naye ili aondolewe.

Wabunge hao wamewaambia waandishi wa habari, leo jijini Dodoma kuwa kitendo kilichofanywa na Spika Ndugai ni uamuzi wake ambao hauna baraka za Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo inajumuisha pia wabunge wa upinzani.

Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amesema uamuzi wa kutangaza kuwa hawawezi kufanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad hauwezi kukubaliwa kwani mwelekeo wake hauna tija kwa Taifa.

Mnyika ambaye alikuwa msemaji kwa niaba ya wenzake leo jumatano, Januari 16, 2019, amesema kambi ya upinzani wanapinga uamuazi huo na wataendelea kuupinga wakihoji hofu aliyonayo Spika hadi atangaze kutofanya kazi na CAG.

“Kwanza ni kwa nini (Spika) asisubiri kwanza CAG aitwe na Kamati ya Maadili ahojiwe juu ya kauli yake ndipo ajue cha kumfanya, lakini yeye ameamua kwenda mbali zaidi na kuzuia kufanya kazi na taasisi nzima ambayo ni jicho la Bbunge na Watanzania,” amesema Mnyika.

Kwa mujibu wa Mnyika, kamati hizo zimezuiwa kufanya kazi yoyote kuanzia Januari 14 hadi 25, 2019 muda ambao walikuwa wanatakiwa kukutana na CAG na kukamilisha ripoti zao ili ziwasiliswe bungeni.

Mbunge huyo ametaja kile alichokiita kuwa ni hofu kwa Serikali kutokana na msimamo wa CAG wa ukweli na uwazi ambao alisema umekuwa mwiba kwa baadhi ya watawala duniani.