Warioba amkumbuka Mrema kwa kuachia uwaziri

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

Muktasari:

Warioba amesema Mrema aliamua kuacha nafasi ya Waziri baada ya kutofatiana na wenzake jambo alilosema siyo dogo katika siasa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema Marehemu Augustino Mrema atakumbukwa kwa mambo mawili ikiwemo kuachia nafasi ya uwaziri baada ya kutofautina na wenzake katika baraza la Mawaziri.

Pia amesema atakumbukwa kwa namna alivyoleta upinzani wa kweli wa kisiasa alipohamia NCCR Mageuzi.

Ameyasema hayo leo Agosti 22 alipozungumza na waandishi wa habari ikiwa ni muda mfupi tangu atoe pole kwa familia ya Mrema katika nyumba yao iliyopo Salasala jijini Hapa.

Mrema alifariki dunia Jumapili ya Agost 21, 2022, saa 12.15 asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam na anatarajiwa kuzikwa Alhamisi hii Mkoani Kilimanjaro.


Warioba amesema Mrema aliamua kuacha nafasi ya Waziri baada ya kutofatiana na wenzake jambo analolitafsiri kuwa si dogo.

"Si wengi waliopata vyeo wakiona kuwa imani yake haiendani na wenzie anaweza kuachia cheo," amesema Warioba.

Jambo la pili alieleza kuwa Mrema ndiye mtu aliyesaidia kuweka msingi wa siasa ya vyama vingi katika nchi.

Amesema alipoondika CCM kwenda upinzani alitoa upinzani wa kweli na kufanya uchaguzi wa kwanza kuwa wenye ushindani.

"Nafikiri kwa sababu ya uwezo aliokuwa nao na mvuto aliokiwa nao, chama alichokuwa kikiongoza cha NCCR Mageuzi katika uchaguzi wa kwanza kilipata vitu vingi vya ubunge baada ya CCM," amesema Warioba.


Katika uhai wake amewahi kushika nyadhifa mbalimbali Serikalini ikiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani.

Pia enzi za uhai wake, mwanasiasa huyo aliwahi kuwa mgombea urais kupitia NCCR-Mageuzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 baada ya kujiunga na chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mrema aliwahi pia kuwa Mbunge wa Temeke kupitia NCCR, hata hivyo aliuacha baada ya kuhamia TLP, ambako pia aliwahi kuwa Mbunge wa Vunjo na hadi amefikwa na mauti alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole.

Mrema ameacha mke na watoto watano ambapo watatu kati yao ni wanaume.