Warioba: Wanasiasa lindeni misingi ya uhuru, amani

Waziri Mkuu, mstaafu Jaji Joseph Warioba akizungumza katika mdahalo wa wanasiasa na wadau wa siasa ulioandaliwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwenyekiti wa taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema viongozi wa vyama vya siasa nchini wana jukumu la kuhakikisha wanalinda misingi ya amani na uhuru iliyowekwa na waasisi wa Taifa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema viongozi wa vyama vya siasa nchini wana jukumu la kuhakikisha wanalinda misingi ya amani na uhuru iliyowekwa na waasisi wa Taifa.

Warioba amebainisha hayo leo Jumanne Septemba 20, 2022 wakati wa kongamano la tathmini ya shughuli zinazofanywa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere tangu kuanzishwa kwake miaka 25 iliyopita.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuwaunganisha wananchi badala ya vyama vya siasa kuwagawa kwa itikadi ya vyama. Jaji Warioba amedai kwamba vyama vya siasa vimekuwa chanzo cha kuwagawa wananchi.

"Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 wa mfumo wa vyama vingi kule Zanzibar watu waligawanyika na ilifika hatua ya kususiana. Ilichukua muda kuwaunganisha.

"Sasa ifike wakati tufanye jitihada kama walizozifanya Zanzibar kwa viongozi wote wa kisiasa kukubali kulinda misingi iliyowekwa ya uhuru wa nchi na wananchi, amani na umoja na amani ya nchi. Wakikubali hilo wote tutafanya kazi ya kuwaunganisha wananchi” amesema.

Warioba ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya ameongeza kuwa, " tuache hizi tabia ya vyama vya siasa kuwagawa wananchi. Viongozi wetu walikuwa mstari wa mbele kuweka misingi ya umoja na amani”.