Washauri jinsi ya kujibana bei za bidhaa zikipaa

Muktasari:

  • Kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita, bei ya baadhi ya bidhaa ilikuwa ikipanda, hasa mafuta ya kula na sukari, lakini mafuta yamekuja kusababisha vitu vingi viwe havishikiki.

Kwa zaidi ya miaka miwili iliyopita, bei ya baadhi ya bidhaa ilikuwa ikipanda, hasa mafuta ya kula na sukari, lakini mafuta yamekuja kusababisha vitu vingi viwe havishikiki.

Serikali imejitahidi mara kadhaa kuwataka wafanyabiashara kutopandisha bei kiholela, lakini vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine vilivyoanza Februari 24, vimesababisha bei ya mafuta kupanda duniani, hivyo nchini pia.

Kupanda kwa bei ya mafuta sio tu kumesababisha nauli za mabasi ya mikoani na daladala zipande, bali ile ya bajaji, bodaboda hata teksi nayo imeenda juu.

Kupanda kwa nauli kumepandisha gharama za usafirishaji na sasa sio vyakula pekee, ila bidhaa za viwandani nazo hazishikiki, jambo lililopandisha gharama za maisha.

“Mimi napenda kununua vitu kwa jumla, lakini bei niliyoikuta leo dukani sijaamini macho yangu. Boksi la sabuni ya mche ya Jamaa tulikuwa tunanunua Sh35,000 ambayo ilipanda ikafika Sh45,000, lakini leo nimeambiwa ni Sh70,000. Siwezi kununua. Nitakuwa nanunua ya kipande mpaka itakaposhuka,” alisema Anna Michael, mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Sio sabuni tu, hata unga wa sembe sasa hivi anasema unauzwa Sh1,200 kwa kilo moja baada ya kuuzwa chini ya Sh1,000 kwa muda mrefu.

Akiwa bungeni, mapema Februari, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza wafanyabiashara nchini kuacha kupandisha bei ya bidhaa za ujenzi kiasi cha wananchi kushindwa kuzimudu na kueleza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa watakaobainika.

Majaliwa ameyasema hayo alipojibu swali la Mbunge wa Msalala (CCM), Iddi Kassim aliyehoji msimamo wa Serikali kuhusu mfumuko wa bei za vyakula, yakiwamo mafuta, sabuni na vifaa vya ujenzi kama nondo, saruji na mabati.

“Kumejitokeza kupanda kwa bei hata kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ambao wakati mwingine ni wa makusudi unaofanywa na wafanyabiashara wasiowaaminifu. Serikali italifanyia kazi kupitia taasisi zake,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu alisema hayo siku chache baada ya Februari 8, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji kuwaagiza wazalishaji, wasambazaji na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi pamoja na vinywaji baridi kushusha bei.

Serikali yalia na saruji

Pamoja na juhudi zote zilizofanywa, bado bei ya bidhaa nyingi haishikiki na juzi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alikutana na kampuni zinazozalisha saruji kuzungumza nazo kuhusu gharama zao za uzalishaji ili kuleta nafuu kwa wananchi pamoja na Serikali inayohitaji saruji kwa ajili ya miradi ya kimkakati inayoendelea kujengwa maeneo tofauti.

Waziri alizungumza na viongozi wa kampuni ya Afrisam ambayo ni mwanahisa mkubwa wa kiwanda cha Tanga Cement.

“Rai yetu, haya mambo ya bei kuongezeka yanaendelea, hasa baada ya kuja hili jambo jipya la vita vya Urusi na Ukraine, tuendelee kukabiliana na majanga ya namna hii huku tukiwajali wananchi masikini. Sisi huku kwenye sekta ya uzalishaji tukichoka kubeba mzigo, wananchi wetu ambao ni watumiaji wa mwisho watachoka zaidi,” alisisitiza Dk Mwigulu.

Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa AfriSam, Erick Diack alisema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 1.2 kwa mwaka na katika kipindi kifupi kijacho wanakusudia kuongeza uwekezaji kuongeza ufanisi kwa kufunga mitambo mingine yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha.

Wataalamu washauri

Kwa hali inayoendelea, kumekuwa na maoni tofauti yanayoweza kumsaidia mwananchi wa kawaida kuishi katika kipindi hiki kigumu huku akiendelea kukidhi mahitaji yake.

Mchumi na Mratibu wa Shahada za Juu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDBS), Dk Diana Mwiru anasema ni muhimu kila mwananchi kuchukua hatua za kukilinda kidogo alichonacho.

Ili kupata nafuu ya jumla, hata wafanyabiashara nao anashauri wapunguze kiasi cha faida wanachopata badala ya kutaka kunufaika zaidi, huku wengi wakiumia. Kama walikuwa wanapata faida ya asilimai 40, anapendekeza waishushe mpaka 25 inayotosha kulinda biashara zao.

“Sio mbaya kutumia inferior goods (bidhaa zenye thamani ndogo) kama inawezekana. Mfumuko wa bei umekuwa changamoto, Serikali iangalie uwezekano wa kutoa ruzuku, hasa kwenye bidhaa muhimu zitakazoufanya uchumi uendelee kukua,” anasema Dk Diana.

Iwapo bei zitaendelea kupanda, anasema baadhi ya wazalishaji watashindwa kuzalisha hivyo kuingia kwenye mdororo wa uchumi.

Msomi huyo anawataka wachumi kuishauri Serikali kuchukua hatua mapema, kwani kwa hali ilivyo ni tofauti na ilivyokuwa nyuma.

“Mfumuko ulikuwa wa tarakimu moja, hata kama mishahara haikupanda lakini watu walikuwa na uhakika wa kupata bidhaa muhimu. Sasa hivi vitu havishikiki, mishahara ambayo haijaongezeka haitoshi tena,” anasema Dk Diana.

Mkurugenzi wa Shahada za Juu wa Chuo cha Usimamizi wa Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema kwa wenye mshahara au kipato kinachofahamika ni vyema wakahakikisha wanakidhi kwanza mahitaji ya lazima kabla ya kufanya sterehe au mambo yasiyo na tija.

“Watu waepuke starehe na matumizi mengine yasiyo ya lazima. Ni muhimu pia kwa Serikali kudhibiti bei, kwani baadhi zinapanda bila sababu ila ukiuliza unaambiwa mafuta,” anashauri mchumi huyo.

Dk Deogratius Mahangira, mhadhiri wa masuala ya kodi UDBS, anasema licha ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, watu wanaweza kubadili mtindo wa maisha kuendana na mfumuko wa bei uliopandisha gharama za maisha.

“Kama nyumbani kuna nafasi, unaweza kupanda mboga badala ya kila kitu kwenda kununua sokoni. Kwenye gari binafsi unaweza kupanga kubeba abiria watatu au wanne watakaochangia mafuta kidogo na ikishindikana sio mbaya kupanda daladala,” anashauri Dk Mahangira.

Kipindi hiki, anakumbusha kuwa ni muhimu sana kuongeza chanzo cha mapato, kwani kupanda kwa bei kunakoshuhudiwa ni hali itakayodumu kwa muda mrefu.

Wananchi nao wafunguka

Kuna hizi sherehe za harusi na sendoff au kitchen party, tunapaswa kuwa nazo makini kwani mambo yamebadilika sana.

“Yaani usipokuwa makini ukahakikisha umenunua mahitaji muhimu kwanza, kuipata hela nyingine ni shughuli. Napendekeza watu wa kumbi za sherehe na vitu vinavyohusiana na hivyo wangepunguza bei zao ili hata michango ya ipungue,” anasema Yosepher Kumburu, mjasiriamali jijini Dar es Salaam.

John Kandeo, mfanyabiashara wa kuku eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam anasema gharama za usafiri zimepanda kwa kiasi kikubwa na hilo ni eneo ambalo Serikali inaweza kuliangalia kwa upekee.

Sio nauli za daladala na mabasi ya mikoani pekee zilizopanda, kwani hata bajaji na bodaboda nazo zimeongezeka, hivyo kuwaumiza wafanyabiashara wenye mtaji mdogo kama yeye.

“Miaka ya nyuma, ulikuwa unaweza kununua pikipiki mpya kwa Sh1.2 milioni, lakini sasa inakaribia moja. Kwa hali ilivyo, watu binafsi watashindwa kuendesha magari yao hivyo bei ya pikipiki na bajaji ikipunguzwa nauli inaweza kushuka. Bodaboda wanaopewa pikipiki kwa mkataba ndio wanaosababisha nauli ipande kutokana na malengo waliyowekewa,” anasema Kandeo.

Ukiacha kupunguza bei ya pikipiki au bajaji, anapendekeza kushushwa kwa gharama za kufunga mfumo wa gesi asilia kwenye vyombo vya usafiri, hasa wa umma kwani ni jambo linalowezekana ili kutoa unafuu kwa wananchi.

“Natakiwa kuzunguka kwa wafugaji kukusanya kuku kuanzia alfajiri. Siwezi kufunga mfumo wa gesi kwenye gari langu ingawa natamani kufanya hivyo, lakini gharama zake ni kubwa sana. Mizunguko yangu ni kila siku…pakiwa na unafuu nitafunga,” anasema Kandeo akieleza kuwa siku asiyotumia gari lake analazimika kukodi.