Wasomi wamwomboleza Profesa Nkunya

Wednesday July 21 2021
wasomi pic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Kufuatia kifo cha Mwenyekiti wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Mayunga Nkunya, wasomi wameeleza kuwa taifa limepoteza mwanasayansi mahiri na mtaalam wa kutegemewa barani Afrika wa mifumo ya udhibiti ubora wa elimu na uendeshaji vyuo vikuu.
Profesa Nkunya ambaye alikuwa Katibu Mtendaji wa kwanza wa TCU baada ya kubadilishwa kutoka baraza la vyuo vikuu alikutwa na umauti mchana wa Julai 21 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mamia ya waombolezaji walijitokeza katika ukumbi wa Nkurumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kumuaga mwanazuoni huyo ambaye pia aliwahi kuwa mhadhiri, mkuu wa kitivo cha sayansi na naibu makamu mkuu taaluma.
Akimzungumzia Profesa Nkunya, Katibu Mtendaji wa TCU Profesa Charles Kihampa alisema kifo chake ni pengo kubwa kwa taifa kutokana na ujuzi aliokuwa nao katika uendeshaji wa mifumo ya elimu ya juu.
Alisema chini ya uongozi wa Profesa Nkunya akatika Baraza la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki litengeneza mifumo ambayo iliunganisha program zinazotolewa kwenye vyuo vikuu Afrika Mashariki hatua inayowezesha mwanafunzi kuhama na kozi yake anapohamia nchi nyingine ndani ya jumuiya hiyo.
“Alitengeneza benchmarks (misingi) ambazo kwa sasa zinafanya vyuo vyote Afrika Mashariki vinatoa watu wanaofanana katika misingi ya kielimu na siku zote alisimamia ubora wa elimu inayotolewa kwenye vyuo vikuu katika nchi hizi za Afrika Mashariki.
“Alikuwa pia mtaalam aliyetumiwa na Unesco, hapa mwishoni alikuwa akitengeneza mifumo ya udhibiti ubora katika nchi mbalimbali za bara la Afrika. Kuna nchi ambazo hazina mifumo kama ambayo tunayo TCU, alishaanza kuwasilisha maandiko katika hizo nchi ila ni bahati mbaya ametuacha kabla haijakamilika,”alisema Profesa Kihampa
 Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Padre Charles Kitima alisema Profesa Nkunya alikuwa na maono ya kutaka vijana wengi wa Tanzania wapate elimu ya juu.
“Akiwa katibu mtendaji wa TCU aliwezesha kuanzishwa kwa vyuo vikuu vingi binafsi ili kutoa fursa kwa vijana wengi wa kitanzania kupata elimu ya juu. Siku zote alitaka elimu ya juu ya Tanzania iko kwenye viwango vya juu,”alisema Padre Kitima.
Kwenye upande wa kemia Profesa Nkunya alitajwa kama mwalimu wa watalaam wa kemia na dawa zinazotokana na mimea wakiwemo waliotengeneza dawa maarufu nchini za Covid19 ikiwemo Covidol na Nimricaf.

Advertisement