Wataalamu wabuni programu wazazi kufuatilia maendeleo ya wanafunzi shuleni

Friday November 26 2021
New Content Item (1)
By Mariam Mbwana

Dar es Salaam. Kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao shuleni baadhi ya wahandisi wa mawasiliano wamebuni programu inayomuwezesha mzazi kufuatilia maendeleo ya ya mtoto shuleni na kupata taarifa mbalimbali za shule kupitia simu ya mkononi.

Taarifa hizo ni pamoja na matokeo ya mtoto kwenye kila somo, kiasi cha ada anachodaiwa mzazi, ratiba ya mwanafunzi shuleni, pamoja na matukio mbalimbali ya shule kwa mwaka.

Mbali na hilo pia inawarahisishia walimu katika kuandaa ripoti za wanafunzi na kuwafikia wazazi kwa urahisi.

Akizungumza katika uzinduzi wa programu hiyo ya Shulesoft, Ofisa Mwandamizi Mkuu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Semo Mwakiyanjala amesema kuwa mfumo huu wa digitali utawezesha taasisi mbalimbali za kielimu nchini kuratibu shughuli zao mbalimbali bila ya kutumia karatasi.

“Mfumo huu utawasaidia kwa kiasi kikubwa wazazi kuwa karibu na watoto wao kitaaluma vilevile kuongeza mapato ya shule husika,”amesema. 

Naye Mkurugenzi wa Shulesoft, Ephrahim Swilla amesema wazo la kubuni program hiyo lilikuja baada ya kufanya tafiti mwaka 2016 katika shule mbalimbali za binafsi na za Serikali na kugundua kuwa kuna changamoto ya mawasiliano kati ya mzazi na shule.

Advertisement

“Kutokana na mawasiliano kati ya mzazi na shule ni muhimu kwa maendeleo ya mwanafunzi tukaamua kuja na program hii ili kuwa daraja kati ya shule na mzazi ili ,”amesema.

Amesema hadi sasa shule takribani 700 zimeshajiunga katika mfumo huo hapa nchini pia vilevile baadhi ya shule kutoka nchi nyingine kama vile Madagasca, China pamoja na UK.

Ameongezea kuwa kupitia mfumo huo mwalimu mmoja ana uwezo wa kuandaa ripoti za watoto wengi kwa kutumia muda mfupi na hufika kwa mzazi kwa haraka zaidi.

Amesema mbali na hiyo mfumo huo utasaidia shule kupunguza upotevu wa mapato ya shule kutokana na tabia ya wanafunzi kula ada kwani kila inapolipwa ada ya mwanafunzi husika mzazi hupata ujumbe kupitia simu yake ya mkononi.

Naye mwakilishi kutoka shule ya Sekondari Canossa, Theresia Paul amesema tangu walipojiunga katika mfumo huo wazazi wamekuwa wakifatilia kwa ukaribu maendeleo ya watoto wao.

“Kwa mfano mzazi anapopata ujumbe wa mazoezi ya mtoto wake kuna somo hafanyi vizuri sana anafika shule kwa haraka kujadili na mwalimu ni kwa namna gani wanaweza kumsaidia mwanafunzi huyo kufanya vizuri,”alisema.

Advertisement