Wataka sheria ya ubakaji kwa wanandoa

Dar es Salaam. Mjadala wa mume kumbaka mkewe jana ulikuwa ni miongoni mwa hoja za wanaharakati wa masuala ya kijinsia baada ya kushauri marekebisho ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 ili kumuwajibisha mume.

Sheria hiyo kwa sasa inatamka kwamba ni kosa la jinai kumlazimisha mwanamke kufanya tendo la ndoa bila idhini yake.

Hata hivyo, wanaharakati hao wameshauri pia kitendo cha mume kumbaka mkewe kitambuliwe kama kosa la jinai katika sheria hiyo kutokana na changamoto ya kukithiri matukio hayo kwenye ndoa.

Pendekezo hilo ni miongoni mwa hoja zaidi ya 30 zilizowasilishwa na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) mbele ya wajumbe wa Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha mfumo wa haki jinai nchini.

Msingi wa mapendekezo hayo unaakisi uamuzi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwateua wajumbe hao 11 chini ya Mwenyekiti Jaji Mohamed Othman Chande Januari 6, mwaka huu kwa lengo la kukusanya mapendekezo ya wadau ili kuimarisha mfumo wa haki jinai katika taasisi tano za Serikali.

Tume hiyo itawajibika kuchambua na kushauri maboresho katika Jeshi la Polisi, Mahakama, Ofisi ya DPP, Magereza, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Uhamiaji.

Tawla ndio ilianza kuwasilisha maoni yake jana kabla ya mtandao wa asasi 182 za kiraia zinazohusika na huduma za usaidizi wa kisheria(TAPNET) na baadaye Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT).

Lightness Raimos, Ofisa Sheria wa Tawla aliieleza tume hiyo kuwa, kitendo cha mume kulazimisha mke kufanya mapenzi bila idhini ni ubakaji kama ilivyo ubakaji mwingine na matukio hayo yameendelea kuongezeka kwa kasi.

“Kwa wiki tunapokea zaidi ya kesi 15 zenye sura tofauti ya ukatili, zaidi zinahusisha malalamiko ya wanawake kulazimishwa kufanya tendo la ndoa, huo ni ubakaji, lakini pia kuna kesi nyingi za kuingiliwa kinyume na maumbile, kwa hiyo ni tatizo kubwa linalohitaji kudhibitiwa,” alisema Lightness.

Maoni mengine ya chama hicho ni kuimarisha mazingira ya faragha katika madawati ya jinsia, kuongeza ujuzi wa maofisa wa madawati hayo pamoja na mashauri ya mtoto kusikilizwa chini ya muktadha wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2019.

“Mtoto hata kama ameua, si bado anahesabika mtoto kwa umri? Kwa mfano panya road tumeshauri ahesabike kama mtoto, sheria yake ipo sio kwamba tunamtetea, changamoto ni jamii ukizungumzia panya road, vinginevyo itengenezwe sheria inayomuondoa kwenye utoto,” alisema Lightness.


Polisi jamii

Kundi la pili kuwasilisha hoja zake 15 lilikuwa ni TAPNET mbele ya wajumbe hao ikiwamo hoja ya kufumua na kusuka upya mfumo wa Jeshi la Polisi nchini.

Katika mabadiliko hayo, mtandao ulishauri uratibu wa kundi hilo la polisi jamii uhamishiwe Serikali za mitaa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki hatua inayopunguza imani ya wananchi kwa jeshi hilo.

Anthony Isakwi, Mratibu wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria wa Jamii Wilaya ya Kinondoni alisema polisi jamii wamechangia kwa kiwango kushiriki matukio ya ukiukwaji wa maadili, unyanyasaji wa raia katika matukio mbalimbali.

“Polisi jamii sasa hivi wanatoa huduma vituo vya polisi, matokeo yake malalamiko yamekuwa mengi sana juu yao, kwa hiyo Serikali za mitaa ziwasimamie hao polisi jamii pamoja na ulinzi shirikishi,”alisema Isakwi.

Pia, mtandao huo ulipendekeza kufumua na kusuka upya pia Tume ya Kuratibu Uthibiti wa Dawa za Kulevya Tanzania (DCC) kwa madai ya kunusuru nguvu kazi inayothirika wa dawa za kulevya nchini.

“Jeshi la Polisi limekuwa likilalamikiwa sana, tumeshauri kufumua mfumo wote na kuangalia maeneo yote kuanzia hatua za mchujo wa kumpata askari ili kuweka misingi ya weledi,” alisema Isakwi.


Majaji, mahakimu

Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) kilishauri kuongezwa kwa makosa yanayohitaji dhamana ili kutekeleza dhana ya mtu kutokuonekana na hatia mpaka itakapothibitishwa na mahakama.

Makamu wa Rais wa JMAT, Shaibu Mzanda alitaja makosa yanayohitaji dhamana kwa sasa ni utakatishaji fedha haramu, rushwa, usafirishaji dawa za kulevya, kukutwa na nyara za Serikali, uhalifu wa kimitandao na uhujumu uchumi, isipokuwa yanayohatarisha usalama wa Taifa kama vile uhaini na ugaidi.

Pia, chama hicho kimeshauri uundwaji wa jukwaa la haki jinai kama inavyoelekezwa chini ya kifungu cha 27 cha Sheria ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) ili kuratibu, kuchunguza na kufuatilia haki ikitendeka.

JMAT pia ilishauri kundwa kwa jukwaa la haki jinai kama inavyoelekezwa na NPS ambayo majukumu yake ni kuratibu masuala yote ya haki jinai na kuchukua hatua pale zinapokiukwa.