Watakaokaidi kuvaa maboya kukiona Sheria ya faini, kifungo jela mbioni kutungwa

Muktasari:

  • Viongozi na watendaji wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Emmanuel Ndomba wanatekeleza kampeni ya kuelimisha wamiliki na abiria katika vyombo vya usafirishaji ndani ya Ziwa Victoria umuhimu wa kuvaa maboya ya kujiokoa wakati wa ajali na majanga.

Geita. Serikali inakusudia kutunga sheria itakayomlazimisha abiria katika vyombo vya usafirishaji majini kuvaa maboya ya kujiokoa  kupunguza vifo wakati wa ajali na majanga.

Akizungumza na wadau wa usafirishaji majini katika mialo ya Nkome, Ujaluoni, Makatani na Runazi wilayani Geita leo Januari 16, 2021, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli nchini (Tasac), Emmanuel Ndomba amesema sheria hiyo itatoa adhabu ya faini na kifungo jela kwa wamiliki na abiria kama ilivyo kwa vyombo vya usafirishaji kwa ya barabara.

"Kuvaa ambavyo sheria inawabana wasifunga mikanda kwenye magari; ndivyo pia inavyotakiwa  kwa wanaosafiri majini," amesema Ndomba

Amesema kwa sasa, sheria inawabana wamiliki pekee kwa kutakiwa kuhakikisha vyombo vyao vinakuwa na maboya kulingana na idadi ya abiria; lakini hakuna uwajibikaji kwa abiria anayekaidi kuvaa maboya..

"Nia ya Serikali ni kuona hakuna anayepoteza maisha  hata pale ajali zinapotokea majini. Na njia ya kufikia lengo hilo ni wamiliki wa vyombo,  wafanyakazi na abiria wote kuzingatia kanuni za usalama kabla ya kuanza na wakiwa safarini," amesema Ndomba 

Kuhusu shughuli za uokoaji wakati wa ajali na dharura, mtendaji Mkuu huyo wa Tasac amesema tayari Serikali inatekeleza mpango wa kujenga vituo sita vya uokoaji ndani ya Ziwa Victoria kikiwemo kituo Kikuu cha uratibu kitakachojengwa jijini Mwanza.

Ujenzi wa vituo hivyo ambavyo pia vitajengwa  katika nchi za Kenya na Uganda zinazomiliki sehemu ya Ziwa Victoria utagharimu zaidi ya Sh4.2 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB

Akizungumzia vifo vinavyotokana na ajali za majini, mmoja wa abiria aliyekutwa katika mwalo wa Ujaluoni, Bundala Lubinzagula ameiomba Serikali kuharakisha mpango wa kutunga sheria inayolazimisha siyo tu uvaaji wa maboya, bali pia bima kwa abiria na vyombo vya usafirishaji majini.

"Kama ilivyo kwa magari, vyombo vya usafirishaji majini pia viwe na bima ya ajali kuwezesha waathirika kulipwa fidia," amesema Lubinzagula

Scolastica Malongo, mmoja wa abiria aliyekuwepo mwalo la Nkome aliiomba Serikali kuhakikisha maboya ya watoto yanakuwepo katika vyombo vya usafirishaji majini huku akihoji kwanini abiria katika vivuko vya Serikali na watu binafsi hawavai maboya