Watalii 150 kutoka Israel watua KIA leo

Kiongozi wa watalii kutoka nchini Israel Shlomo Carmel akipokea zawadi ya Ua  baada kufanikisha ujio wa watalii kutoka Israeli ,kulia Mkuu wa mkoa Arusha John Mongela na Mwenyekiti wa bodi ya Utalii Jaji mstaafu Thomas Mihayo. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Watalii 150 kutoka Israel wamekuja nchini, ikiwa ni sehemu ya watalii wengine 900 wanaotarajiw akutua nchini.

Arusha. Kundi la watalii 150 kutoka nchini Israel limetua uwanja wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) leo Agosti 2 saa 10:30 alfajiri kwa ajili ya kutembelea hifadhi za taifa.


Watalii hao ni sehemu ya watalii 900 ambao wanatarajia kutua nchini mwezi huu kutembelea vivutio vya utalii.


Akizugumza baada ya kupokea watalii hao Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema ujio wa watalii hao ni kutokana na kazi nzuri ya kutangaza utalii inayofanywa na serikali na wadau wa utalii.


"Leo tumepokea kundi la kwanza la watalii hawa ambao wanakuja nchini kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na janga la Corona," amesema RC Mongela.


Kiongozi wa watalii hao, Shlomo Carmel ameipongeza Tanzania na ukarimu mkubwa ikiwepo kuwapokea alfajiri.


Mwenyekiti wa bodi ya Utalii, Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema ujio wa watalii hawa ni sehemu ya watalii zaidi ya 900 watakaokuja nchini mwezi huu.


"Tumefurahi kuanza kuwapokea Hawa watalii na wanakuja baada  kujiridhisha na hatua za serikali katika kupambana na ugonjwa wa Ugonjwa wa Corona kwendana na matakwa ya shirika la afya la umoja wa mataifa (WHO) na mashirika mengine," amesema.


Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mawasiliano wa shirika la hifadhi za Taifa (TANAPA), Pascal Shelutete amesema ujio wa watalii hawo ni jitihada kubwa za kutangaza Utalii  katika masoko mapya, ikiwepo Israel ambayo imechangiwa pia na serikali kufungua ubalozi nchini humo.


"Tumekuwa tukijitangaza sana kuvutia watalii na haya ni sehemu ya mafanikio katika soko hili jipya la Israel kwani mwaka jana pia tulipokea zaidi ya watalii  1000," amesema Shelutete.


Shelutete amesema watalii hao watatembelea hifadhi za kaskazini na Mamlaka ya hifadhi Ngorongoro.


Amesema baada ya kufika nchini watalii hawa tahadhari zote za afya zitachukuliwa kuanzia uwanjani hadi hifadhini ili kuhakikisha watalii wanaingia salama nchini na kutoka salama.