Watano wadakwa wakidaiwa kuiba mbuzi, ng’ombe mkoani Pwani

Muktasari:

  • Wafanyabiashara watano wa nyama mjini Kibaha wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za wizi wa mbuzi na ng’ombe wenye thamani ya zaidi ya Sh50 milioni.

Kibaha. Wafanyabiashara watano wa nyama mjini Kibaha wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za wizi wa mbuzi na ng’ombe wenye thamani ya zaidi ya Sh50 milioni.

Mifugo hiyo  iliibiwa juzi Jumatatu Mei 10, 2021 eneo la Tangini Muheza mjini na kijana aliyekuwa akichunga mifugo hiyo, George Mtiganda hakurudi nyumbani.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani,  Wankyo Nyigesa amesema leo Jumatano Mei 12, 2021 kuwa walikamata zaidi ya kilo 235 za nyama ya ng'ombe porini zilizopangwa kuuzwa kwenye mabucha saba yaliyopo Picha ya Ndege, Loliondo, Kiluvya kwa Komba, Kwa Mathias  na Mailimoja.

"Juzi tulipokea taarifa ya kuibiwa ng'ombe 25 pamoja na mbuzi 31 mali ya Rajabu Maulid (69) mkazi wa Dar es Salaam, siku ya tukio mifugo hiyo ilikuwa na kijana huyo.”

"Tulianza msako na tukabaini kuna nyama iliyochinjwa porini na kusambazwa kwenye mabucha siku iliyofuata..., tulikuta nyama kwenye mabucha saba na waliokuwa wakiuza katika mabucha hayo tuliwakamata ila mmiliki wa maduka hayo amekimbia,” amesema.

Kwa upande wake Maulid amesema siku ya tukio saa 1 usiku alipata taarifa kuwa aliyekuwa akichunga mifugo yake hakurudi nyumbani na kwa kuwa alikuwa jijini Dar es Salaam aliomba msaada kwa majirani zake waliomsaidia kutoa taarifa polisi.