Watanzania kufaidika na kampeni ya lishe

Mwakilishi Mkazi wa FAO,  Dk Nyabenyi Tipo, Mkuu wa Mali asili wa EU,  Lamine Diallo wakishuhudia upandishaji wa bendera kuashiria uzinduzi Mradi wa Lishe Jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

Mradi huo utakaogharimu Sh1.34 trilioni unalenga kuboresha lishe, kukuza uzalishaji wa kilimo na kuongeza kipato cha wakulima wadogo.

Dar es Salaam. Zaidi ya Watanzania 32 milioni watafaidika na kampeni ya lishe inayolenga kuimarisha lishe na biashara ya mazao ya kilimo.
Mradi huo unaojulikana kwa jina la Agri-Connect umefadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na kutekelezwa na Shirika la Kilimona Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO).
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo jijini hapa, Mkurugenzi wa Taifa wa Usalama wa Chakula, Dk Honest Kessy aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo, alisema licha ya Tanzania kujitosheleza kwa chakula, bado asilimia 35 ya wananchi wana utapiamlo.
“Tanzania inajitosheleza kwa chakula asilimia 120, lakini asilimia 35 ya Watanzania wamedumaa. Pia kuna ongezeko la unene name uzito uliopitiliza unaosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kikiwemo kisukari,” alisema Dk Kessy.
Amesema kampeni hiyo imekuja kwa wakati ambao dunia inapambana na maambukizi ya Uviko-19 na hivyo kuboresha kinga dhidhi ya ugonjwa huo.
“Kuondoa utapiamlo ni kipaumbele cha Serikali ya Tanzania. Tumeimarisha miongozo ya lishe kwa kuhamasisha uwekezaji zaidi katika kilimo, uzalishaji wa chakula na elimu ya lishe ili kuongeza upatikanaji na ufikikaji wa ulaji kiafya na kupitia uzalishaji wa kilimo,” alisema.
Kwa upande wa mwakilishi mkazi wa FAO, Dk Nyabenyi Tipo alisema; “Wakati janga la dunia likiendelea umuhimu wa lishe kudhibiti athari zake ni muhimu.”
“Mabadiliko ya jamii katika uzalishaji wa chakula, matumizi na masoko yataongeza upatikanaji wa chakula, kuongeza kinga za mwili na kuongezea wakulima wadodo kipato,” alisema Dk Tipo.
Naye Mkuu wa Maliasili wa Umoja wa Ulaya nchini, lamine Diallo alisema kilimo na lishe ni pande mbili za sarafu zinazotakiwa kuendelezwa ili kuongeza uzalishaji wa kilimo kutokana na ongezeko la idadi ya watu duniani.
“Tanzania inaweza kupambana na tatizo la utapiamlo kama itatilia maanani wa uzalishaji wa kilimo. Tunaamini kampeni hii ikiunganishwa na malengo ya Agri-connect itaonganisha wadau na kuhamasisha ukuaji wa afya na utajiri wa watu,” alisema Diallo.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum anayehamasisha lishe, Neema Lugangira alisema kampeni hiyo itawawezesha Watanzania kukabiliana na matatizo ya afya kabla ya kuhitaji huduma za hospitali.
“Mara nyingi matatizo ya utapiamlo yamekuwa yakiratibiwa na Wizara ya Afya, wakati ambao tayari mtu anakuwa ameshapata madhara. Lakini Wizara ya Kilimo inakuwa kabla ya mtu hajapata madhara, kwa hiyo kampeni hii itawezesha wananchi kujua umuhimu wa lishe kabla ya kupata madhara,” alisema.