Watanzania washauriwa kuchangamkia biashara mitandaoni

Muktasari:

  • Watanzania wametakiwa kuchangamkia biashara za mitandaoni kutokana na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano inayowezesha upatikanaji wa bidhaa kwa urahisi duniani kote.

Dar es Salaam. Watanzania wametakiwa kuchangamkia biashara za mitandaoni kutokana na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano inayowezesha upatikanaji wa bidhaa kwa urahisi duniani kote.
Hayo yameelezwa  mwishoni mwa wiki na mkufunzi chuo cha masoko na mauzo wa chuo cha Access cha jijini Dar es Salaam, Peter Msechu aliyebainisha kuwa biashara ya mtandao ina fursa nyingi katika soko la Tanzania.
“Kulikuwa kuna kampuni kama Jumia ambayo ilikuwa ikifanya vizuri kwenye biashara ya mtandao,” amesema akisisitiza kuwa kuna takribani Watanzania milioni 23 wanaotumia mtandao na  wana uwezo wa kutumia mtandao kufanya manunuzi na kukuza soko la biashara ya mtandao.
Amesema hata hivyo, mwishoni wa mwaka 2019, Jumia ilisitisha shughuli zake nchini akidai kuwa huenda hata manunuzi kupitia njia ya mtandao yameshuka ama kupungua kabisa.
“Jumia ambayo ilikuwa biashara  ya mtandao nchini haipo tena ikiwaacha Watanzania wengi wa manunuzi ya mtandaoni bila huduma hiyo. Takribani asilimia 15 ya watu nchini wanatumia intaneti hivyo kuna wanunuzi wengi wa njia ya mtandao (online),” amesema Msechu.
Mbali na Jumia, Msechu anaitaja kampuni ya Q-net akidai nayo imeonekana kufanikiwa katika masoko ya mtandao ikifanya mauzo ya moja kwa moja ikionekana kuziba pengo la Jumia.
“Ni kweli, biashara ya mtandao nchini Tanzania bado iko katika hatua ya maendeleo, hata hivyo bila shaka inauwezo wa kukua haraka,” alisema
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ambapo Watanzania wanatilia shaka uendeshaji wa biashara hiyo.
“Kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao bado ni tatizo na ndiyo changamoto iliyofanya Jumia kuondoka nchini,” amesema.
Msechu ametoa sababu ya biashara ya mitandaoni kushamiri akisema ni pamoja na kuzuka kwa magonjwa yanayoambukiza kutokana na mikusanyiko hasa Corona.
 
Pia amegusia suala la miundombinu akisema kukosekana kwa miundombinu bora hasa kwa maeneo ya mijini  kunaongeza haja ya ufanyikaji wa bishara ya mitandaoni.
Ameitaja pia kampuni ya The Mall of Africa iliyopo nchini Nigeria akisema ni soko la mtandaoni lililojipanua Afrika Magharibi, huku kampuni za Alibaba inaongoza Afrika na Kilimall nchini Kenya akisema ni mifano ya masoko hayo ya mitandaoni.
“Tanzania ikiwa katika hatua za kupunguza umaskini kwa kuboresha maisha, na idadi kubwa ya watu wakiwa wanaishi vijijini, biashara ya mtandao inayowezesha watu kuuza na kununua moja kwa moja inatoa suluhisho hilo.”
“Kimsingi, uuzaji wa moja kwa moja hutumia fursa ya kuuza bidhaa na huduma moja kwa moja kwa watumiaji, popote walipo,” amesema.
Amesema  kama yaliyo mashirika mengine, katika biashara mtandaoni mteja huagiza bidhaa mtandaoni kupitia mshirika ambae huwasilisha bidhaa hizo.
“Hii inafanya biashara kuwa urahisi kwa pande zote mbili yaani mnunuzi na muuzaji. Kupitia biashara ya mtandao, wafanyabiashara wanapata fursa ya kuuza na kuongeza mauzo ya bidhaa zao na kuwafanya wanunuzi kupata huduma kwa viwango vya kimataifa,” amesema.