Watatu kortini kwa kumteka Hussein
Muktasari:
- Kabla ya kuteka, washtakiwa hao wanadaiwa kumtishia kwa bastola, mfanyabiashara Hussein na kisha kumuibia simu aina ya Iphone.
Dar es Salaam. Wakazi watatu wa Morogoro wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shtaka moja la unyang'anyi wa kutumia silaha na kumteka mfanyabiashara.
Washtakiwa hao ni Sufian Kidevu (30) mkazi wa Kizuka mkoani; Celestini Kamuli (32) mkazi wa Kizuka na mfanyabiashara Husein Mwinyijuma (47) mkazi wa Gairo Magengeni, wote wanatoka mkoani Morogoro.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo, Mei 29, 2023 na kusomewa shtaka lao na wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ferdinand Kiwonde.
Wakili Mwanga amedai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 85/2023.
Akiwasomea shtaka hilo, wakili Mwanga amedai washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 17, 2023 katika Mtaa wa Zaramo na Jamhuri eneo la Posta jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa siku hiyo ya tukio, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuiba simu moja ya mkononi aina ya iPhone, mali ya Hussein Mohamed.
Kabla ya kutenda kosa hilo, washtakiwa wanadaiwa kumtishia Husein kwa bastola aina ya Luger yenye namba A712040 ili waweze kutekeleza wizi huo.
Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka lao walikana kutenda kosa hilo.
Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Kiwonde aliahiridha kesi hiyo kutokana na shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
"Shtaka la unyang'anyi wa kutumia silaha mnalokabiliwa nalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo mtaendelea kuwa rumande," amesema Hakimu Kiwonde.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 12, 2023 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.
Hali ilivyokuwa:
Tofauti na washtakiwa wengine wanaofikishwa katika Mahakama ya Kisutu ambao huonekana kirahisi, washtakiwa hao walifichwa mahabusu iliyopo mahakamani hapo na baadae walipandishwa mahakamani kwa kupitia mlango wa ndani ambao hutumiwa na askari Magereza pamoja na washtakiwa wa ndani hadi ukumbi namba moja ulipo ghorofa ya kwanza katika mahakama hiyo.
Wakiwa ndani ya mahakama hiyo, muda wote washtakiwa hao walikuwa wameinamisha nyuso zao chini hadi pale waliposomewa shtaka lao.
Ulinzi waimarishwa
Kabla ya kusomwa kwa kesi hiyo ulinzi uliimashwa katika mahakama hiyo hasa sehemu ambayo washtakiwa walikuwa wamehifadhiwa (Mahabusu).
Washtakiwa hao walikuwa chini ya ulinzi mkali wa zaidi ya askari saba waliokuwa wanawalinda ambao walikuwa wamevaa kiraia na wengine wakiwa kwenye share, huku baadhi yao wakiwa na silaha.
Walipoingizwa kwenye mahakama ya wazi, ulinzi ulikuwa mkali zaidi, huku watu wakizuiliwa kuingia isipokuwa waandishi wa habari.
Walisomewa shtaka lao wakiwa kwenye ulinzi mkali na walipomaliza kusomewa walirudishwa kupitia mlango wa ndani ya mahakama hiyo.