Watatu wahukumiwa kunyongwa kwa mauaji

Muktasari:

Watu watatu wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji, akiwemo aliyemuua mtoto wa mke wake baada ya kumkuta mama yake anatumia vidonge vya kupunguza makali ya ukimwi (ARV).

Tabora. Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, imewahukumu kunyongwa hadi kufa watu watatu waliokuwa wanakabiliwa na kesi mbili tofauti za mauaji, akiwemo aliyemuua mtoto wake baada ya kumkuta mama yake mzazi akimeza vidonde vya kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV).

Waliohukumiwa ni pamoja na Haruna Ndayanze mkazi wa kijiji cha Pozamoyo wilayani Kaliua na Ally Shaban na Ally Mtoni Kambogo wakazi wa kijiji cha Igalula Wilaya ya Uyui mkoani Tabora.

Hukumu hiyo imetolewa leo Desemba 8 na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Tabora Demetrio Nyakunga aliyekasimiwa mamlaka ya ziada ya kusikiliza mashauri ya mahakama kuu.

Katika shauri la kwanza mahakama hiyo, imemuhukumu kunyongwa hadi kufa Haruna Ndayanze baada ya kumtia hatiani kwa kumuua Kusaga Magulu aliyekuwa mtoto wa mke wake aliyezaa na mwanaume mwingine.

Upande wa mashitaka ukiwakilishwa na mawakili Mwerito Ukongoji na Sabrina Silayo, uliiambia mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 25, 2020 katika kijiji cha Pozamoyo wilayani Kaliua.

 Imedaiwa kuwa siku hiyo mshitakiwa alitimiza nia hiyo ovu kwa kumkata kata kwa panga shingoni, mikononi na mwilini mtoto huyo.

Upande wa mashitaka ambao ulileta mashaidi 12 uliiambia mahakama hiyo kuwa, sababu za mauaji hayo ni kutokana na mshitakiwa kumkuta mkewe, Stephania Alphonce, akimeza vidonge vya kufubaza virusi vya Ukimwi.

Katika shauri la pili, pia Hakimu Nyakunga amewahukumu kunyongwa hadi kufa Ally Shaban Kinyogoli na Ally Mtoni Kambongo baada ya kuwakuta na hatia ya kumuua Ally Rajabu mkazi wa kijiji cha Igalula Wilaya ya Uyui.

Upande wa mashitaka uliiambia Mahakama hiyo kupitia kwa mashahidi wanane kuwa, washitakiwa walitenda kosa hilo Machi 22, 2020.

Katika shauri lingine, mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Tabora, imemwachilia huru Zengo Kulwa mkazi wa kijiji cha Izugawima wilaya ya Uyui, aliyekuwa akituhumiwa kwa kosa la kumua Joseph Elias, hata hivyo ushahidi haukutosha kumtia hatiani.