Watoto 113 wadakwa wakidaiwa kuwa wahalifu

Watoto 113 wadakwa wakidaiwa kuwa wahalifu

Muktasari:

  • Watoto 113 wamekamatwa na polisi  mkoani Tabora kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu ukiwemo wa unyang'anyi wa kutumia silaha.

Tabora. Watoto 113 wamekamatwa na polisi  mkoani Tabora kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu ukiwemo wa unyang'anyi wa kutumia silaha.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Safia Jongo amesema watoto hao 17 wamekamatwa Wilaya ya Nzega na 96 wamekamatwa Wilaya ya Tabora katika operesheni maalum ya kupambana na uhalifu lengo likiwa ni kufanya mkoa wa Tabora uwe salama.

"Watoto wamekuwa ni changamoto kubwa katika mkoa wa Tabora kwani wanaojihusisha na uhalifu wengine wakishirikiana na watu wakubwa,” amesema.

Ameeleza kuwa baadhi ya watoto waliokamatwa wenye umri wa kuanzia miaka minane hadi 15 wamekiri kufanya vitendo vya uhalifu ambavyo mbali ya upigaji na ukataji mapanga pia wamekuwa wakipora simu za watu.

Amewataka wazazi na walezi kuchukua jukumu la kuwatunza na kuwalinda watoto wao dhidi ya uhalifu na kwamba ataendelea na operesheni za kuwasaka watoto wahalifu kwani ni tatizo kubwa mkoani Tabora hasa Wilaya za Nzega na Tabora.

Kamanda Jongo ameeleza makundi ya uhalifu ya watoto yamekuwa yakijioachika majina mbalimbali yakiwemo ya Roho mbili na Roho Saba na kuwa ana matumaini Polisi watawadhibiti watoto hao.

Imeandikwa na

Robert Kakwesi,mwananchi