Watoto 96 hubakwa kwa mwaka Ludewa

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Andrea Tsere amesema ukatili wa jinsia bado ni tatyizo kubwa wilayani humo, kwani takwimu zimeonyesha wastani wa watoto 96 wamekuwa waakibakwa kwa mwaka.

Ludewa. Mkuu wa Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Andrea Tsere amewataka wananchi kupiga vita imani za kishirikina na ukatili wa kijinsia, akisema takwimu zimeonyesha wastani wa watoto 96 wamekuwa wakibakwa wilayani humo kila mwaka.

Akizungumza leo Desemba 9, 2022 katika maadhimisho ya siku ya uhuru wilayani hapa, Tsere amekemea vitendo vya ukatili wa jinsia akisema bado ni tatizo kubwa.

“Kwa taarifa niliyo nayo watoto watano mpaka wanane wanabakwa kila mwezi, jumla watoto wanaobakwa kwa taarifa niliyo nayo ni watoto 96 kwa mwaka tena watoto wachini ya miaka mitano jambo hili sio zuri ni lazima tulipige vita vikali,” amesema Tsere.

Lakini pia amewaasa wananchi kutoa taarifa pale wanapo shuhudia vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kukomesha tabia hiyo.

“Kipigo chochote kinavunja na kupoteza amani katika jamii yetu, hivyo ni jukumu letu wote kukemea vikali suala hili na tutoe taarifa katika vyombo husika kwaajili ya msaada wa kuwanusuru wa hanga wa ukatili huu.

“Wanawake wengi wanapigwa huo nao ni uvunjifu wa Amani. Wapo na wanaume wanaopigwa lakini inabaki siri ya ndani, tupige vita ukataili wa kijinsia kwani ni moja ya sababu za uvunjifu wa amani.” amesema Tsere.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ludewa, Monica Mchilo ametaja imani za kishirkina kuwa moja ya moja ya sababu za ukatili wa kijinsia.

“Kwa kiasi kikubwa ukatili wa kijinsia unafanywa humu mitaani unachagizwa na imani za kishirikina, kwa sababu huwezi ukawa unampiga tu mkeo au mmeo kila siku.

“Ukiangalia taarifa ya Mkuu wa Wilaya amesema watoto watano mpaka nane wanabakwa kila mwezi, kwa mtu mwenye timamu hawezi fanya hili jambo lazima kuna sababu nyuma inayo msukuma kufanya hivyo,” amesema Mchilo.