Watoto wanne wafa baada ya nyumba kuungua Simanjiro

eneo ambako nyumba imeungua na kusababisha vifo vya watoto wanne katika Kijiji cha Ngage Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Watoto wanne wamefariki dunia baada ya nyumba yao kuungua moto uliosababishwa na petroli katika Kijiji cha Ngage Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Simanjiro. Watoto wanne wamefariki dunia baada ya nyumba kuungua moto wakiwa ndani katika Kijiji cha Ngage Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Mei 4, 2022, Diwani wa Kata ya Loiborsoit, Siria Kiduya amesema tukio hilo limetokea jana mchana.

Kiduya amesema ajali hiyo pia imejeruhi mtu mmoja ambaye ni bibi wa watoto hao waliofariki.

Amesema kuwa watoto watatu walifariki papo hapo huku mmoja akifariki baada ya kupelekwa hospitalini.

"Watoto watatu walifariki dunia papo hapo na bibi akajeruhiwa na mtoto mwingine walipelekwa hospitali ya KCMC ya Moshi Mkoani Kilimanjaro," amesema Kiduya.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni bibi huyo, Anna Kipututu kutumia petroli ili kuwaua kunguni waliokuwa kwenye kitanda chao.

Amesema baada ya bibi wa watoto hao kumwagia petroli katika kitanda aliwasha moto ili kuwaua kunguni na moto ukaunguza nyumba wakiwa ndani.

Mkuu wa wilaya ya Simanijiro, Dk Suleiman Serera amethibitisha vifo hivyo na kutoa pole kwa wananchi wa kijiji hicho.