Watoto watatu walioteketetea moto Rombo wazikwa kaburi moja

Majeneza yaliyobeba mabaki ya miili ya watoto watatu wa kiume wa familia moja walioteketea kwa moto katika kijiji cha Lessoroma wilayani Rombo ikiwa kwenye kaburi moja. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Watoto hao watatu waliteketea kwa moto baada ya nyumba yao kuungua katika Kijiji cha Lessoroma wilayani Rombo wamezikwa leo Januari 25 katika kaburi moja.

Rombo. Mamia ya waombolezaji waliokuwepo kwenye mazishi ya watoto watatu wa kiume walioteketea kwa moto katika Kijiji cha Lessoroma wilayani Rombo wamejikuta wakiangua vilio baada ya mama mzazi wa watoto hao Karesma Theodory 29 kuongea maneno ya uchungu wakati akiwaga wanaye.
"Wanangu mmeniacha na nani, mbona mmeondoka wote mkaniacha mwenyewe, nitamtuma nani tena wanangu, nitaongea na nani uwiiii," haya ni baadhi ya maneno yaliyowaliza wengi katika mazishi hayo.
Watoto hao ambao ni Erick (9) Joshua (7)na Gidion Theodory (2) walifariki dunia kwa ajili ya moto na miili yao kuteketea usiku wa  Januari 21, 2023 wakati mama yao akiwa hayupo huku chanzo cha moto  huo kikielezwa kuwa walikuwa wakichezea kibatari.

Akizingumza wakati wa ibada ya mazishi, Paroko wa Parokia ya Usseri, Amedeus  Mtui amewataka waombolezaji waliokuwepo kwenye mazishi hayo kuiweka kwenye maombi familia hiyo kutokana na wakati mgumu walionao na kuitaka jamii kuacha kuzungumza maneno mengi juu ya tukio hilo na kwamba yote yaliyotokea kwani ni mapenzi ya Mungu.
"Hilo jambo kibinadamu ni zito, lakini Mungu ndiye aliruhusu haya yatokee kwa hiyo tunampa sifa na shukrani kama Ayubu alivyofanya hata katika yote yale aliyopitia hakumkufuru Mungu, wapo watu waliomshawishi lakini aliendelea kusimama imara," amesema.
"Kwa hiyo niwatie moyo familia, msikate tamaa, tuwaombeeni hii familia, tuungane pamoja maana haya majaribu kibinadamu ni magumu na sisi tutaendelea kuwatia moyo familia katika kipindi hiki kigumu kwenu," amesema.
Evaristi Silayo, Mwakilishi wa Mbunge wa Rombo,  Profesa Adolf Mkenda aliitia moyo familia hiyo na kwamba ofisi yake itaendelea  kushirikiana na familia kwa hali na mali kuona namna ya kuisaidia familia ikiwemo kushirikiana na familia kujenga nyumba nyingine kwenye eneo ambao liliungua na moto.
"Mbunge wenu anawatia moyo, yupo katika majukumu mengine ya kiserikali na amenielekeza nimwakilishe kwenye mazishi haya, lakini amepokea kwa masikitiko makubwa msiba huu na ameahidi familia, kwamba baadaye ataangalia utaratibu wa namna ya kushirikiana na familia na wananchi kuona namna ya kurejesha  nyumba hapa palipoungua kwa moto," amesema.
Watoto hao wamezikwa leo katika kaburi moja nyumbani kwao katika Kitongojj cha Kitefure Kijiji cha Lessoroma, wilayani Rombo.