Watoto wawili wafariki baada ya kuzama mtoni
Muktasari:
- Watoto wawili waliofahamika kwa jina la Revocatus Beatus (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Isanzu na mdogo wake Japhet Beatus (7) anayesoma chekechea, wamefariki dunia mara baada ya kuzama mtoni.
Mwanza. Watoto wawili waliofahamika kwa jina la Revocatus Beatus (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Isanzu na mdogo wake Japhet Beatus (7) anayesoma chekechea, wamefariki dunia mara baada ya kuzama mtoni.
Akitoa taarifa ya tukio hilo kwa waandishi wa habari leo Disemba 8, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema tukio hilo limetokea saa tisa alasiri Desemba 6 mwaka huu wakati wawili hao wakichunga Ng'ombe.
"Tukio hilo lilitokea wakati watoto hao wakichunga Ng'ombe ndipo mtoto Japhet aliacha Ng'ombe na kwenda kuogelea pembeni ya mto Butindo, ambapo alizidiwa na maji ya mto huo, ndipo kaka yake Revocatus kuamua kwenda kumuokoa,” amesema na kuongeza;
“Hata hivyo, maji yaliwazidi nguvu, na watoto wote wawili walizama na kupoteza maisha. Wakazi wa eneo hilo wanadai kuona Ng'ombe wakiwa hawana Mchungaji, waliamua kufuatilia ndipo wakagundua watoto hao wamezama.”
Hata hivyo Kamanda Mutafungwa ametoa wito kwa wananchi kuzidi kuchukua tahadhari kubwa kutokana na hali ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
"Kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, naomba wazazi na walezi kuongeza usimamizi wa karibu kwa watoto, wasicheze kwenye mito, mabwawa au maeneo mengine hatarishi,” amesema kamanda huyo na kuongeza;
“Pia tunawaomba viongozi wa vitongoji, mitaa na kata kuendelea kutoa elimu ya tahadhari na madhara ya mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali."