Watu 48 wakamatwa tuhuma za utapeli, kupora Moro

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa wakati akitoa taarifa za matukio mbalimbali ya uhalifu. Picha na Lilian Lucas.

Muktasari:

Watu 48 wanashikiliwa na Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za utapeli wa kuuza viwanja zaidi ya mara mbili

Morogoro. Watu 48 wanashikiliwa na Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo za utapeli wa kuuza viwanja zaidi ya mara mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Mei 25, 2022 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslim amesema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya operesheni maalumu kufanyika katika mkua huo.

Amesema kuwa katika tukio la kwanza watu 16 wamekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na utapeli wa kuuza viwanja kwa mtu zaidi ya mmoja maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

 Amesema watu hao walikuwa wakighushi nyaraka na kugonga mihuri bandia katika nyaraka mbalimbali ili kutekeleza uhalifu wao.

“Hawa watu wamekuwa wakishirikiana na viongozi mbalimbali wasio waadilifu kwenye maeneo yao na walikuwa wakipima viwanja katika mashamba yasiyokuwa yao, wanaandaa mihtasari feki na hati bandia za umiliki na uuzaji,”amesema.

Kamanda huyo amesema kuwa watuhumiwa hao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya watendaji wa taasisi, mamlaka na idara mbalimbali za Serikali katika kutanda uhalifu huku wakiwa kero na kuzua taharuki katika jamii ambapo kunapelekea kuweza kutokea kwa uvunjifu wa amani.

Amesema Polisi inaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine waliotoroka au kuhama huku akiwataka kujisalimisha.

Katika tukio la pili kamanda Muslim vijana 25 wenye umri kati ya miaka 16 hadi 21 wanashikiliwa kwa tuhuma za kujihusisha na kucheza kamari katika mapagale na nyumba mbovu usiku.

Amesema katika tukio la tatu linawahusisha wapanda pikipiki (bodaboda) saba maarufu kama Vishandu kukamatwa kwa kujihusisha na wizi wa simu kwenye maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro.

Kamanda Muslim alisema wapanda bodaboda hao wamekamatwa maeneo ya Msamvu mzunguko, standi ya Dodoma, Ipoipo, Mkundi, Chamwino, Nanenane, Modeko, Kihonda na Masika.

Pia Kamanda huyo amesema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani kwa hataua zaidi za kisheria.