Watu 50 hutibiwa magonjwa ya afya ya akili Bugando kwa siku

Watu 50 hutibiwa magonjwa ya afya ya akili Bugando kwa siku

Muktasari:

  • Uongozi wa  hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando umesema kwenye kliniki zake za nje  inahudumia wagonjwa wenye matatizo ya akili kati ya 30 hadi 70 kwa siku.

Mwanza. Uongozi wa  hospitali ya rufaa ya Kanda ya Bugando umesema kwenye kliniki zake za nje  inahudumia wagonjwa wenye matatizo ya akili kati ya 30 hadi 70 kwa siku.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya magonjwa ya afya ya akili duniani yanayofanyika katika hospitali hiyo mkuu wa idara ya afya ya akili katika hospitali hiyo, Dk Kiyetia Hauli amesema kutokana na uhitaji wa matibabu hayo wamelazimika kuongeza kliniki za magonjwa hayo kutoka tatu hadi tano kwa wiki.


Dk Haule amesema wagonjwa wawili hadi sita wanalazwa katika kitengo cha afya ya akili kila siku kutokana na hali zao kuhitaji matibabu na uangalizi maalum.


"Wagonjwa wa ndani wamekuwa wakipewa huduma siku zote za wiki ambapo kwa siku wagonjwa wawili hadi sita wanalazwa katika kitengo cha magonjwa ya afya ya akili huku kukiwa na vitanda 50 vya kulaza wagonjwa wao," amesema Dk Haule.


Daktari bingwa  wa afya ya akili kwa watoto na vijana, Dk Gema Simbee amewataka wazazi na wakazi wa Kanda ya Ziwa kujenga desturi ya kufanya uchunguzi wa magonjwa ya afya ya akili kwa watoto ili kuwahi matibabu pale wanapogundulika kuwa na magonjwa hayo.


Ameongeza kwamba asilimia 50 ya magonjwa hayo huwapata watoto wakiwa tumboni hadi umri wa miaka 14 kwa kuwa magonjwa hayo ni ya kurithi.


Ametaja baadhi ya dalili za magonjwa hayo kwa watoto kuwa ni watoto kufanya vitu hatarishi, kutokuwa na utulivu, kukosa uelewa wa kutaaluma darasani, kukaidi maelekezo ya nyumbani, kukosa uwezo wa kujihudumia wenyewe, kujikondesha kutokana na ulaji hafifu, utukutu, kushindwa kumudu kujihudumia na kunyanyasa watoto wenzao.


"Ukiachilia mbali dalili hizo kuna visababishi ya magonjwa hayo ambavyo ni homa kali ya degedege, changamoto za uzazi, kushindwa kuhudhuria kliniki ipasavyo, lishe duni kwa mama na mtoto, magonjwa ya mwili na kuumia sehemu ya kichwa kutokana na ajali," amesema Simbee


Mkazi wa Wilaya ya Bunda mkoa wa Mara, Anna Kizito amesema tangu aanze matibabu ya afya ya akili mwaka 2014 anajisikia vizuri huku akitoa wito kwa jamii kuepuka mila potofu ya kwenda kwa waganga wa kienyeji wanapougua badala yake waende hospitalini ili kupatiwa matibabu ya kitaalam.